skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Matinde Nestory, Mwanza

Taasisi za umma na binafsi zilizopo mkoani Mwanza zimetakiwa kuunga mkono mchakato wa sensa kwa kuhamasisha wananchi Kushiriki katika zoezi hilo linalotarajia kufanyika Aug 23 mwaka huu.

Rai hiyo imetolewa na katibu tawala Mkoa wa Mwanza Ngussa Samike wakati akizungumza kwenye kikao na viongozi wa kamati ya Amani kutoka madhehebu ya kiislam na kikristo katika ukumbi wa Mwanza hoteli jijini Mwanza.

Bw. Samike ameeleza kuwa Taasisi hizo na viongozi wa dini washiriki kwa kuweka jumbe za matangazo kwenye nyumba za ibada kwa kuwapa elimu waumini juu ya sensa na kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa kwa kushirikiana na makarani wa sensa.

Samike amesema lengo la sensa ya watu na makazi ni kupata taarifa sahihi za kidemografia, kijamii, kiuchumi na hali ya mazingira kwa lengo la kupata takwimu zitakazowezesha Serikali na wadau wengine kupanga maendeleo ya watu katika sekta muhimu za afya,Elimu,Nishati na Madini,Miundo mbinu na maji Safi.

“Sensa ya watu na makazi ni moja ya zoezi muhimu linalokusanya taarifa za Kila mtu aliyelala ndani ya mipaka ya nchi taarifa hizi zitahusu Kidemografia, taarifa za Kilimo Mifugo Uvuvi na Misitu,taarifa za Uzazi,Ulemavu, Elimu, taarifa za Kiuchumi,huduma za kijamii pamoja na anwani za makazi”amesema Samike.

Ameongeza kuwa umuhimu wa sensa hauishii serikalini unaenda mpaka kwenye ngazi ya chini kwa jamii ambao viongozi wa dini wanaziongoza.

“Nawapongeza Sana kwa jitihada ambazo mmefanya, sisi tunapopoke Wito wowote kutoka kwa viongozi wa dini tuko tayari katika ngazi ya Mkoa nawapongeza kwa ushirikiano ambao mkonao kuanzia katika ngazi ya uongozi wenu mpaka katika ngazi za chini huu ushirikiano mlionao  na serikali tunashukuru Sana”amesema Samike.

Kwa upande wake Askofu Charles Sekerwa amesema sensa itasaidia kujua idadi ya watu, maendeleo, mikakati na ubora wa uongozi.

“Sisi Kama viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali ya kikristo na kiislam tupo bega kwa bega na Raisi wetu tunaahidi tutakuwa mabarozi wazuri kwa kuwahimiza waumini wetu Kushiriki vyema katika zoezi Zima la sensa ya watu na makazi” amesema Askofu Sekerwa.

Nae Sheikhe Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke amesema tumeshaanza kuelimisha waumini wa dini zote juu ya sensa ya watu na makazi tumetembea wilaya zote za mkoa wa Mwanza kuelimisha waumini katika zoezi Zima la sensa.

“Tulishaanza kuelimisha Jambo hili lakini tukaona bado sisi ni namba mbili maana wewe ulituelimisha sisi na sisi tunawaelimisha wenzetu tukaona ni vizuri kamati ya amani kutafuta uwezekano wowote ili tuje kuwaita viongozi wetu na wewe uje uzungumze nao”amesema Sheikhe Kabeke.

Kwa upande wake mratibu wa sensa wilaya ya Nyamagana  Ruhinda Costantine amesema kuwa sensa ya watu na makazi ni ya sita kufanyika nchini Tanzania.

Ameongeza kuwa  sensa hiyo itahusisha makarani wa sensa ambao watatembea kaya zote nchini na kufanya mahojiano na Mkuu wa kaya ambao watawasaidia kupata takwimu sahihi ili kukamlisha zoezi hilo.

This Post Has 0 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma