skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Asema ni mpango wa kumtua mama kuni kichwani , Amshukuru Rais Samia

Na. Mwandishi wetu

Wanawake mama lishe, baba lishe na makundi maalumu ya kijamii wapatao 400 wakazi wa jimbo la Kasulu Mjini mkoani Kigoma leo wamegawiwa majiko ya gesi safi ya kupikia kama sehemu ya mpango wa taifa wa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ulioasisiwa Novemba mosi 2022 na Rais wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan

Akikabidhi majiko hayo mbunge wa Jimbo la Kasulu mjini ambaye pia ni Waziri wa Nchi, ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na wenye ulemavu Profesa Joyce Ndalichako amesema ugawaji huo wa majiko ni utekelezaji wa mpango wa taifa wa kuwatua kuni kichwani wanawake na kuhamasiha matumizi ya nishati mbadala

Prof. Ndalichako amebainisha kuwa jumla ya ya wajasiriamali wanawake na wanaume mia nne (400) wananufaika na mpango huo mjini Kasulu ikiwa ni awamu ya kwanza katika utekelezaji huo ambao unawalenga mama lishe na baba lishe.

Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na wananchi na wanufaika wa mpango wa majiko ya gesi mjini Kasulu

Mama Samia Rais wetu aliwezesha wabunge wote kupata angalau majiko 100 ya gesi kama sehemu ya hamasa na mimi nikalibeba suala hili kwa uzito wake kwa kutafuta nyongeza ya majiko mengine 300 ili kusaidia wapiga kura wangu hasa wanawake kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa, kwahiyo leo ninawatua kuni wanawake wenzangu na hata wanaume ambao wanajihusisha na biashara ya mapishi katika kata zote za jimbo langu”. Amesisitiza Profesa Ndalichako

Majiko hayo hayo yenye thamani ya shilingi milioni 30 yametolewa katika makundi mbalimbali yakiwemo ya wanawake mama lishe, baba lishe watumishi katika halmashauri ya Mji, shule zote za msingi na sekondari Pamoja na shirikisho la walimu mjini Kasulu.

Akitoa shukurani kwa niaba ya wanufaika wote Mwalimu Hamisa Juma Rajabu ambaye ni mkuu wa shule ya sekondari Kidyama ameweka bayana kuwa msaada huo wa majiko ya gesi ni chachu ya ukuaji wa uchumi kwa jamii, na yatachochea ari ya watumishi wa umma wakiwemo walimu kupata kifungua kinywa sehemu za kazi bila kuharibu misitu.

Akihutubia mamia ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Profesa Ndalichako ameweka bayana kuwa, jamii nchini imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa nishati safi ya kupikia na hivyo kutegemea kuni na mkaa ambao hata hivyo unachangia uharibifu wa mazingira na kuleta athari za kiafya kwa baadhi ya watumiaji hususani wazee na Watoto.

Mwalimu Hamisa ametumia fursa hiyo kumpongeza profesa Ndalichako kwa namna anavyowahudumia wananchi katika jimbo lake na kutaja kuwa misaada mbalimbali anayotoa imegusa kila kundi hususani uchumi, afya na elimu ambapo amefadhili madawati kwa shule za msingi, viti na meza kwa shule za sekodari, cherehani kwa vijana na makundi ya wanawake mafundi wa ushonaji na pikipiki kwa vijana maarufu boda boda.

Mnufaika mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mama Wawili ambaye ni mama lishe ameweka bayana kuwa hajawahi kuona mbunge anayewakumbuka mama ntiliye katika umri wake na kwamba profesa Ndalichako amekuwa wa kwanza kufanya hivyo.

“Sijawahi kuona Mbunge yeyote wa Kasulu aliyekumbuke mama ntilie, wewe ni wa kwanza wengine wanatuona kama si watu wa thamani lakini wewe umetuheshimisha sana, tunakuombea kwa mwenyezi Mungu azidi kukujalia mafanikio Zaidi.

Kwa Pamoja wamempongeza rais Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoshughulikia changamoto mbalimbali za jamii ikiwemo utoaji wa pesa za kutosha kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu, afya na maji nchini na pia kwa kumwamini mbunge wao Profesa Joyce Ndalichako katika nafasi ya Uwaziri.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma