skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameutaka Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kutumia mashirika ya ndege ya Afrika katika usafirishaji wa vifurushi ili kuendelea kuonesha umuhimu wa huduma za posta barani humo.

Amesema hayo leo jijini Arusha, wakati akizindua jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika, hafla iliyoudhuriwa na Mawaziri wanaosimamia Sekta ya Posta kutoka kutoka katika nchi za Liberia, Afrika Kusini, Uganda, Malawi na Tanzania pamoja na wadau wa posta kutoka nje ya Bara la Afrika.

“PAPU ifanye mashirika posta Afrika kusafirisha vifurushi ndani ya Bara la Afrika, sasa posta ilazimishe ndege zetu kusafiri katika nchi za Afrika kupelekea vifurushi. Posta Afrika iwe na maduka ambayo yatawarahisishia wafanyabiashara kufanya shughuli zao”, ameeleza Rais Samia.

Ameongeza “Sina shaka PAPU inaweza kufanya mageuzi makubwa kuleta mabadiliko ya kidijitali katika utoaji wa huduma za posta ndani ya Afrika ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia pamoja na kutimiza mahitaji ya wateja”.

Rais Samia akizindua rasmi jengo jipya na la kisasa la makao makuu ya Posta barani Afrika ambalo limejengwa mjini Arusha nchini Tanzania

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema kuwa Afrika inaweza kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa kufanyabiashara ndani ya bara hilo.

“Ni wakati sasa wa Afrika kufanyabiashara kati ya nchi zetu, ndani ya Bara la Afrika. Na Posta Afrika tupo tayari kuwezesha kuongezeka kwa kiwango cha biashara kati ya nchi za bara hili.

Jengo la PAPU linatajwa kuwa alama muhimu ya umoja na ushirikiano ulipo katika nchi za bara hilo na litasaidia kuboresha utendajikazi wa shughuli za posta kwa mafanikio zaidi.

Aidha, uzinduzi wa jengo hilo ulitanguliwa na mikutano kadhaa iliyohusisha watunga sera, wasimamizi na waratibu wa sekta ya posta kutoka ndani na nje ya Afrika ambapo walijadili masuala mbalimbali ya kuboresha sekta hiyo ikiwemo mafumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma za posta sambamba na kuchangia uchumi za nchi za kiafrika.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma