skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Ashura Ramadhani

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri mkuu Kazi, Ajira, vijana na watu wenye ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Kasulu Mjini Profesa Joyce Ndalichako amekabidhi madawati mia moja (100) yenye thamani ya shilingi milioni nane kwa shule ya msingi Nyansha katika Jimbo la Kasulu mjini kama sehemu ya mkakati wake wa kumaliza kero ya madawati kwa shule zote za mjni Kasulu.

Akikabidhi madawani hayo ambayo yametengenezwa kwa hisani ya Shirika la Posta Tanzania, Prof Ndalichako, ametoa pongezi za moja kwa moja kwenda kwa shirika hilo akitaja kuwa limeunga mkono  juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari, Samia Suluhu Hassan katika sekta ya Elimu kwa kuisaidia madawati hayo  shule ya msingi Nyansha.

Aidha, Prof Ndalichako amewataka wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii kwakuwa Serikali na mashirika mbalimbali wanajitolea sana kwenye sekta ya elimu.

Profesa Ndalichako (kulia) akipokea madawati hayo kutoka kwa Mwakilishi wa posta masta mkuu Bw. Amos Milinga wakati wa hafla ya kupokea na kukabidhi madawati kwa shule ya msingi Nyansha mjini Kasulu. Picha na. Ashura Ramadhani

Juhudi za mbunge huyo pamoja na serikali katika sekta ya elimu ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia pamoja na ujenzi wa shule mpya ambapo katika jimbo la Kasulu mjini shule mpya za msingi zipatazo tano (5), na sekondari sita (6) zinajengwa ili kuhakikisha kila mtoto katika jimbo la Kasulu mjini anapata elimu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Amosi Milinga, kwa niaba ya Posta Masta Mkuu wa shirika hilo, ametoa shukrani za dhati kwa Profesa Ndalichako na uongozi mzima wa jimbo la Kasulu Mjini kutokana na mapokezi yao na kwamba wao kama shirika la posta Tanzania wanaamini kutoa madawati hayo wamesaidia wanafunzi kutimiza ndoto zao.

Bw. Milinga amesisitiza kwamba, mbali ya kukabidhi madawati kwa mbunge pia itasaidia kuboresha  mazingira na miundombinu mingine ili kuongeza kasi ya maendeleo.

Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Izack Mwakisu (kushoto) akipokea madawati hayo kwa niaba ya serikali kutoka kwa Mbunge Prof. Joyce Ndalichako (kulia), wakishuhudiwa na Mwenyekiti wa CCM (w) Bw. Mbelwa Abdallah Chidebwe (mwenye kofia) makamu Mwenyekiti wa halmshauri ya Mji Kasulu Bw. Jonas Selemani (katikati) na Diwani wa kata ya Nyansha Bw. Patrick Madaraka

Mkuu wa wilaya ya Kasulu Mheshimiwa Kanali Izack Mwakisu, amesema mchango huo wa madawati wameupokea kwa mikono miwili,  na msaada wa madawati umepunguza uhaba kutokana na kwamba wilaya hiyo bado unakabiliwa na upungufu wa madawati.

Kambamba na shughuli hiyo, mkuu wa wilaya Kanali Mwakisu ametumia hadhara hiyo kuonya jamii kuhusu Imani za kishirikina kuhusiana na swala la KAMCHAPE, akisema huo ni utaratibu uliowekwa na baadhi ya watu matapeli unaohusiana na mambo ya ushirikina na unapelekea kupunguza heshima katika jamii na kuleta udhalilishaji wa hali ya juu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji Kasulu Bw. Dolla Kusenge, amesema jitihada kubwa za mbunge anazozifanya zinaonekana na kwamba hata yeye zinamsaidia kwa namna moja au nyingine, kwa sababu madawati yakiwepo mashuleni yanatoa nafasi kubwa kujifunza kwa wanafunzi na walimu kufundisha katika mazingira mazuri.

Mbunge wa Kasulu Mjini Profesa Joyce Ndalichako akihutubia wananchi, wanafunzi na walimu baada ya kupokea na kukabidhi madawati 100 kwa shule ya msingi Nyansha mjini Kasulu mkoani Kigoma.

Naye mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi. Telidesa Jonas, amemshukuru Mbunge pamoja na shirika la Posta Tanzania kwa kuwapatia madawati ambayo yamemaliza kabisa changamoto ya wanafunzi kukaa wengi kwenye dawati moja, na kuwaomba kusaidia uboreshaji wa madarasa matano ambayo yangeweza kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.  

Wanafunzi wa shule ya msingi Nyansha, katika shairi lao kwa mgeni rasmi wamewashukuru waliotoa msaada wa madawati kwani umewapa chachu katika usomaji wao, na kuahidi kusoma kwa bidii na kuhudhuria shuleni huku wakieleza kwamba msaada huo utasaidia kutokomeza kabisa utoro shuleni hapo.

Kwa mujibu wa Posta Masta wa wilaya ya Kasulu Bw. Omary Mpamila, madawati yote yametengenezwa na mafundi wa Kasulu kama sehemu ya Posta kuinua kipato cha wenyeji na kurejesha fadhila kwa jamii ambao shirika la posta linawahudumia na anatumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kuzitumia huduma za Posta Tanzania

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma