skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mwandishi wetu, Bukoba

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Ndolage na kuhimiza kiwe kimekamilika ifikapo Novemba 2023 kama walivyoahidi.

“Nimekagua ujenzi wa majengo mapya, naona kazi ni nzuri. Hawa mafundi waendelee na kasi hii na ujenzi ukamilike ifikapo Novemba kama mlivyoahidi ili Desemba, 2023 tuanze usajili wa wanafunzi na Januari, mwakani vijana wetu waanze masomo,” amesema.

Ametoa wito huo leo (Jumapili, Septemba 24, 2023) mara bada ya kukagua uboreshaji wa majengo ya chuo hicho, wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kumpokea katika kijiji cha Bushagara, kata ya Kamachumu, wilayani Muleba, mkoani Kagera.

Amesema katika kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema tuimarishe vyuo vya ufundi stadi nchini ili vijana waweze kupata stadi na kujiajiri. “Chuo hiki kinaweza kuchukua vijana wa ngazi zote hata wa chuo kikuu, hapa wakija wanakuja kupata ujuzi iwe ni wa kuchomelea nondo au kusuka kwani mtu anaweza kuwa na digrii yake lakini hawezi kuchomelea nondo,” amesema.

Amesema Halmashauri nchini zitenge bajeti za kuwasaidia vijana wanaohitimu ili wapate  mitaji ya kuanzia kulingana na stadi walizojifunza.

Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA nchini, Bw. Anthony Kasore alisema Serikali ilitoa sh. millioni 903.5 kwa ajili ya upanuzi wa chuo hicho kwa kuongeza miundombinu ya majengo ili kufikia viwango vya chuo cha wilaya.

“Upanuzi wa chuo unahusisha ujenzi wa mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80; moja la wavulana na jingine la wasichana; bwalo la chakula lenye uwezo wa kuhudumia watu 200; karakana ya umeme; karakana ya uungaji na uundaji vyuma; nyumba ya Mkuu wa Chuo na jiko.”

Alisema mradi huo ulianza kutekelezwa Juni, 2023 na sasa umefikia asilimia 50 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2023. “Upanuzi wa chuo hiki utawezesha kuanza kudahili wanafunzi wa bweni, kwani hivi sasa chuo kinatoa mafunzo kwa wanafunzi wa kutwa pekee, kwa kuwa hakina miundombinu muhimu kama mabweni, bwalo, jiko na nyumba za watumishi.”

Akiwa njiani kuelekea Nshamba, Waziri Mkuu alisimama Kamachumu na kuzungumza na wananchi waliokuwa wakimsubiri njiani. Aliwaeleza miradi inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita na mipango iliyopo ya kuwafikishia huduma katika maeneo yao.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaonya vijana na wanaume wanaokatisha masomo ya wanafunzi wa kike kwa kuwadanganya na lifti za bodaboda.

“Hapa Kamachumu iko changamoto ya wanafunzi wa kike, ndoto zao zinafifishwa. Niwatangazie wanaume: Achana kabisa na matamanio ya mtoto wa kike. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza kwa kumlinda mtoto wa kike, na hii haimaanishi kwamba hamlindi mtoto wa kiume,” alifafanua.

“Rais wetu ametoa fedha nyingi za kujenga shule za sekondari, kwa hiyo Halmashauri tengeni fedha za mapato ya ndani na kujenga mabweni kwani mnao uwezo huo; makusanyo yenu yako juu. Mnakusanya shilingi bilioni saba kwa mwaka, kwa hiyo mkitenga kila miezi mitatu, mtaweza kujenga haya mabweni,” alisisitiza.

Alisema kwa mujibu wa sheria za nchi, mtu akikutwa na kosa la kumpa ujauzito mwanafunzi anastahili kifungo cha miaka 30. “Mwache mtoto wa kike asome kuanzia chekechea hadi chuo kikuu. Mtoto wa mwenzio ni wa kwako, ni mwanao. Siyo mkubwa mkubwa mwenzako,” alisema.

Akiwa njiani kuelekea Magalini kukagua soko la kimataifa la dagaa, Waziri Mkuu aliwasalimia wakazi wa Nshamba na kuwaelezea mpango wa Serikali kusogeza huduma za kijamii kwenye sekta zote.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa kituo cha afya cha Kakunyu kilichopo km. 75 kutoka tarafa ya Bunazi, wilayani Missenyi na kutoa siku tano kiwe kimeanza kufanya kazi.

Muonekano wa Kituo cha Afya Kakunyu ambacho Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kuona maendeleo ya ujenzi wake, Septemba 23, 2023 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Septemba 23, 2023) mara bada ya kukagua kituo hicho, wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kumpokea katika kijiji cha Bugango, wilayani Missenyi, mkoani Kagera.

“Mkurugenzi, hawa madaktari wameletwa kufanya kazi. Watafutie meza, dawa zipo, wape makaratasi yao waanze kuhudumia wananchi. Nakupa siku tano, hapo mapokezi na vyumba vya madaktari vianze kazi sababu hawa tayari wapo hapa kijijini,” amesema wakati akimpa maelekezo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Bw. John Wanga.

Waziri Mkuu alikagua majengo yaliyokamilika ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, wodi ya wazazi na kliniki ya uzazi na mtoto (RCH). Kituo hicho kimegharimu sh. milioni 613 ambapo sh. milioni 523 ni za mapato ya ndani na sh. milioni 90 zilitoka Serikali kuu ambazo zimetumika kujenga nyumba moja ya kuishi watumishi watatu (3 in 1). 

Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi hao kwamba sh. milioni 150 zimekwishatolewa na Serikali ya awamu ya sita ili zitumike kununua vifaa tiba vya kituo chao. Alipoulizwa kuhusu uwepo wa fedha hizo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Isesanda Kaniki alikiri kuwa fedha hizo zimeshapokelewa na zimetumwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili kulipia vifaa tiba hivyo.

Aidha Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wakazi hao wachangamkie fursa za kilimo cha mazao ya chakula na biashara kwa sababu kilimo ni fursa, kilimo ni uchumi  na kilimo ni maisha.

“Endeleeni kulima mazao ya miezi mitatu mitatu kama maharage na mahindi, ili muweze kuuza nchi za jirani. Mheshimiwa Rais alitoa sh. bilioni 50 za ruzuku ya pembejeo hasa mbolea ili mpate mbolea hiyo na kuzalisha zaidi mazao. Jiandikisheni ili mpate namba za kudumu za kielektroniki za utambulisho. Namba hizi zitawasaidia kupata unafuu wakati wa kununua pembejeo,” alisema.

Aidha, aliwataka wakazi hao watunze vyanzo vya maji dhidi ya mifugo na ukataji miti hovyo kwani uharibifu wa vyanzo vya maji ni mkubwa. “Uharibifu ni mkubwa na mifugo mingi ilikuwa inaingia kuja kuharibu vyanzo na sisi wenyewe hatuvilindi. Serikali zote za vijiji na Kamati za Mazingira nenda muwe wakali dhidi ya watu wanaoharibu vyanzo vyetu ili tupate maji mengi kwa ajili ya matumizi ya vijijini, majumbani na mashambani.”

“Wenyeviti wa vijiji na kamati zenu za maendeleo za kata, simamieni eneo la mazingira kwani hali si nzuri. Duniani leo, kuna mabadiliko makubwa ya hali ya hewa, hata majira ya mvua yamebadilika. Kwa nini? Ni kwa sababu tumeharibu vyanzo. Nani ameharibu? Ni sisi wenyewe. Nani atavilinda? Ni sisi wenyewe. Hebu tuvilinde vyanzo vyetu,” alisisitiza.

Waziri Mkuu yuko mkoani Kagera kwa ziara ya siku tatu na leo atazuru wilaya ya Muleba. 

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma