skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Ashura Ramadhan, Kasulu

Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Kasulu kimempongeza Mbunge wa jimbo la Kasulu Mjini Prof. Joyce Ndalichako ambaye pia ni Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na wenye ulemavu kwa namna anavyotekeleza ilani ya Uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2020 kwa vitendo

Pongezi hizo zimetolewa jana na viongozi wa matawi, kata na wilaya ambao walikutana katika kikao cha ndani cha Jimbo la Kasulu mjini katika ofisi za chama ambapo mbunge huyo alitoa taarifa ya miradi inayotekeleza katika eneo hilo.

Katibu wa chama wa wilaya ya kasulu mjini Abdallah Kazwika akiwasilisha pongezi hizo amempongeza mbunge wa jimbo hilo kwani miundombinu iliyoanzishwa kwa asilimia kubwa imekamilika huku mengine ikiendelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu

Nae mmoja wa viongozi wa kata katika jimbo hilo, ameeleza kuwa imani waliyonayo kwa mbunge wao ni kubwa na kumuomba kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kulifanya jimbo la kasulu kuwa na miundombinu madhubuti ikiwemo barabara na maji.

Profesa Joyce Ndalichako akihutubia viongozi wa matawi, kata na wilaya katika mkutano maalumu wa Jimbo la Kaasulu Mjini uliofanyika katika Ukumbi wa CCM mjini Kasulu

Akihutubia katika mkutano huo maalumu wa kijimbo, Waziri Wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu,Kazi, ajira, vijana Na Watu Wenye ulemavu ambae Ni Mbunge Wa Jimbo La Kasulu Mjini Prof Joyce Ndalichako ameweka bayana Maendeleo yanayoendelea kufanyika ikiwemo Miundombinu. Afya, Elimu na Uwezeshaji jamii kiuchumi.

Ametaja baadhi ya miradi inayotekelezwa jimbooni kuwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa na utoaji wa madawati katika shule mbalimbali za msingi na sekondari, Ujenzi wa shule shikizi mpya, ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, ujenzi wa miundombinu ya barabara na mifereji ya maji katika mitaa na usaidizi wa kijamii kwa wazee na watu wasiojiweza kupitia mfuko wa maendeleo TASAF.

Prof Ndalichako amewataka wananchi Wa Kasulu Kuwa Na subira kwani michakato ya kimaendeleo ikiwemo barabara inaendelea kufanyika Na Hivi karibuni itakamilika.

Profesa Ndalichako (kulia) akimsikiliza mmoja wa wajumbe wa mkutano huo aliyekuwa na shida mahususi kwake iliyohitaji ufafanuzi au usaidizi wa Mbunge.

Hata Hivyo ametoa pongezi Kwa Raisi Wa Jamhuri ya muungano Wa Tanzania Dkt .Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyosimamia kikamilifu utekelezaji wa Ilani kwa kutoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo sambamba na namna anavyoiongoza nchi na kudumisha Amani Na utulivu.

Kikao hicho Cha wajumbe Wa CCM Jimbo La Kasulu kimeudhuriwa Na Katibu Wa Chama Wa Wilaya Abdalla Kazwika, Katibu mwenezi Wa Wilaya Joel Maderere Na Katibu Wa Wazazi Ndugu Mapigano.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma