skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mwandishi wetu, Pwani

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameitaka Idara ya Kazi, Ofisi ya Waziri Mkuu kusimamia mpango wa urithishwaji wa ujuzi kwa wazawa kama ilivyobainishwa katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini.

Rais Samia ametoa tamko hilo leo mara baada ya ufunguzi wa kiwanda cha kutengeneza vioo cha Sapphire Float Glass.

Aidha, Rais Samia amesema mpango huu utawasaidia Watanzania wengi kupata ujuzi na ajira na kumsaidia mwekezaji kupunguza gharama za kuajiri wataalamu wa kigeni.  

Vile vile, Rais Samia amesema serikali inaendelea kuwekeza kwenye mifumo ya utoaji huduma ili kupunguza urasimu na kutekeleza hatua za kiuchumi ambazo zimepokelewa vyema na wadau wa maendeleo.

Hali kadhalika, Rais Samia amesema Serikali inatarajia kuzindua Mfumo wa kielektroniki wa kuhudumia wawekezaji (Tanzania Electronic Investment Window) ambao utaunganisha taasisi 12 za serikali zinazotoa huduma kwa wawekezaji.

Rais Samia pia amesema wawekezaji watakaotaka kuwekeza nchini watapewa msaada katika mchakato wa usajili wa kampuni, upatikanaji wa ardhi, vibali na leseni kupitia dirisha moja la huduma ndani ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).  

Rais Samia amehitimisha ziara yake mikoa ya kusini ambapo akiwa njiani kurejea jijini Dar es Salaam amezungumza na wananchi wa Somanga, Ikwiriri na Mkuranga na kuwaeleza nia ya serikali ya kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma