skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akitoa maagizo kwa wataalamu wa afya kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya COVID-19 vinavyosababisha homa ya CORONA. Kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. Pembe na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohammed Janabi.

Baadhi ya wataalamu kutoka Muhimbili Upanga na Mloganzila, MUHAS, JKCI na MOI wakiwa kwenye mkutano.

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Juma Mfinanga akitoa mada kwenye mkutano huu.

Wataalamu wa afya wakimsikiliza mtoa mada kuhusu jinsi ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya COVID-19.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma wa Muhimbili Upanga na Mloganzila, Bw. Aminiel Aligaesha akizungumza na waandishi wa habari juu ya hatua zilizochukuliwa na wataalamu wa taasisi hizo katika kuzuia maambukiziya virusi vya COVID-19.

Baadhi ya ndugu wa wagonjwa wakielekezwa kunawa mikono ili kujikinga kuambukizwa na virusi ya COVID 19 kabla ya kuingia wodi ya Mwaiesela kuwajulia hali.

Wananchi wakinawa mikono getini kabla ya kuingia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Wauguzi wa Muhimbili wakiwaelekeza ndugu jinsi ya kuwaona wagonjwa kwa mpango maalumu.

Askari wakisimamia ndugu wa wagonjwa pamoja na wataalamu wa Muhimbili kunawa mikono kabla ya kuingia Muhimbili.

Utaratibu ukiendelea wa kunawa mikono getini kabla ya ndugu kwenda wodini kuwaona wagonjwa.
Na John Stephen

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH-Upanga & Mloganzila) ikishirikiana na Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Tiba ya Moyo Jakaya Kikwete (JCKI) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) zimeitikia wito wa Mh. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu (MB) na Miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) wa kuchukua hatua mbalimbali za tahadhari ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya COVID 19 vinavyosababisha homa ya CORONA ambapo leo imethibitika kuwepo mgonjwa mmoja nchini Tanzania.

Akingumza na vyombo vya habari, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma, Hospitali ya Taifa Muhimbili Bw. Aminiel Aligaesha ambaye ametoa taarifa maazimio ya kikao hicho kwa niaba ya MNH (Upanga & Mloganzila), MOI, MUHAS, JKCI, amesema Wakuu wa Taasisi zilizomo ndani ya Muhimbili wamekaa na kujadili utekelezaji wa hatua mbalimbali ikiwemo wito na maagizo ya Serikali kuhusiana na kuchuka tahadhari.

“Hatua hizo ni pamoja na kuwataka wafanyakazi, ndugu na jamaa wa wagonjwa wote wanaoingia eneo la Muhimbili kunawa mikono kwa kutumia maji yenye dawa yaliyowekwa katika maeneo mbalimbli ya taasisi hizo kabla na baada ya kuingia ndani ya Hospitali, wodini na sehemu za kutolea huduma” amesema Bw. Aliagesha.

Amesema, taasisi hizo pia zimeunda kikosi kazi kinachoratibu zoezi zima la tahadhari dhidi ya Corona ambacho kinatoa mafunzo kwa wafanyakazi wote wa taasisi hizo, wanafunzi, mafunzo kwa wakufunzi (ToT) watakaosaidia kuelimisha umma kushirikiana na Wizara ya Afya.

Aliongeza kuwa Uongozi wa Taasisi hizi umekubaliana kwa kauli moja kuwa kuanzia sasa wataruhusiwa ndugu wawili tu kwa kila mgonjwa mmoja wakati wa asubuhi na jioni ambapo mchana ni mtu mmoja tu atakayeruhusiwa kupeleka chakula kwa mgonjwa ili kupunguza msongamano mkubwa uliopo eneo la Muhimbili. Tunawaomba wananchi kuunga mkono hatua hizi ili kuongeza tahadhari dhidi ya ugonjwa huu.

Kinga ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya COVID 19 vinavyosababisha homa ya CORONA ni pamoja na kuepuka msongamano, kunawa mikono vizuri kwa maji safi titirika na sabuni, au maji yenye dawa, kutumia vitakasa mikono, kutumia vikinga pua na mdomo (masks), kuepuka kugusana, kukaa mbali na mtu mwenye dalili za mafua na mwenye historia ya kusafiri katika nchi zenye mlipuko wa ugonjwa huo.

This Post Has 0 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma