Na. Irene Bwire -PMO na Anita Balingilaki Buha - Simiyu WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka…
Adela Madyane na Prosper Kwigize -Ujiji Kigoma
Baadhi ya wananchi wanaoishi katika tarafa ya Mwanga Kusini kata ya Kagera, Machinjioni Majengo na Rusimbi wanaoishi karibu na eneo la uwekezaji la Kigoma Special Economic Zone ( KISEZ) wameanza kuvunjiwa nyumba zao huku kukiwa na malalamiko ya kutolipwa fidia kutoka serikalini.
Uamuzi wa kuvunja nyumba hizo umefikiwa baada ya mamlaka za serikali kutoa notisi ya siku 15 iliyotolewa Disemba 31, 2022 ili kuwaandaa wananchi hao kuhama bila shuruti kwa lengo la kupisha uwekezaji na shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kiwanda cha asali, chuo uganga tawi la Muhimbili, pamoja na hospitali ya kanda.
Akiongea wakati wa zoezi la kuvunja nyumba hizo Patric Simeon amesema mbunge wa Kigoma mjini Kirumbe Ng’enda alifika katika eneo hilo na kuwaambia kwamba watafanyiwa uhakiki ili wajulikane wananachi waliolipwa na ambao hawajalipwa kabla ya kuvunja nyumba zao ili kila mmoja apate haki yake lakini wameshangaa kuona hakuna uhakiki wowote uliofanyika na tayari nyumba zimeanza kuvunjwa toka jana.

“Mimi sitahama kwenye nyumba yangu kwakuwa sijalipwa pesa yoyote na sijafanyiwa uhakiki wowote, kama wanakuja kuvunja waje wavunje ila mimi sitavunja nyumba yangu mpaka waje wafanye tathmini kwakuwa wakivunja bila tathmini nitawezaje kulipwa stahiki zangu?” Amehoji Simeon.
Naye Masoud Juma amesema nyumba zimevunjwa bila idhini yoyote ya mahakama na kwamba serikali haikuona haja ya kusikiliza malalamiko yao licha ya kufika katika ngazi mbalimbali za mkoa na taifa kwaajili ya msaada juu ya jambo hilo
“Kila tulipoenda kulalamika hatukusikilizwa, tulipotaka kuandamana na mabango tulikatazwa na kuambiwa tusubiri mwekezaji atakuja kuonana na wananchi lakini cha kushangaza hakuna mwekezaji aliyefika kuongea na sisi na tuliona mabango kwenye nguzo za umeme za notisi ya kuvunja nyumba ndani ya siku 15 na jana wakaja kuanza kuvunja, tumekosa msaada na hatujui tufanye nini” Amesema Juma
Kwa upande wa Method Kifyete baba wa watoto 14 amesema hajui atawaweka wapi watoto wake na kuomba serikali iingilie kati na kuwawezesha kupata eneo la makazi
Akizungumia hilo Mariam Haruna amesema mazingira ni magumu toka walivyovunjiwa nyumba, na kwamba iliwalazimu kulala nje na kupeleka baadhi ya vyomba kwa majirani na huku vingine vikiibiwa na watu wasiokuwa na hofu ya Mungu.
Mwaija Athumani amekiri kuwa wapo waliolipwa pesa za fidia lakini wakaamua kuuza kwa watu wengine ambao hawakuwa na taarifa kwamba eneo hilo ni la uwekezaji na hivyo kuwatia hasara.
Mariam Haruna kutoka kata ya Machinjioni ameiomba serikali kumsaidia kwakuwa yeye ni mjane na hana namna ya kuishi kwakuwa anaye mtoto mmoja wa kike anayemtegemea na mazingira yake ki maisha ni magumu kwani hata kazi anayofanya haiwezi kumuwezesha kupanga au kupata nyumba nyingine

Akizungumzia hilo Deogratius Sangu mkurugenzi mtendaji wa Kigoma Special Econom Zone (KISEZ) amesema changamoto ilyojitokeza ni kwa baadhi ya wananchi wasio waaminfu waliouza maeneo hayo baada ya kulipwa fidia zao na wao kwenda kujenga katika maeneo mengine
“Wapo wananchi wanaoishi maeneo jirani waliovamia maeneo hayo kwakuwa yalipotengwa kuwa eneo la uwekezaji hayakuendelezwa na walipovamia wakayafanya kuwa makazi na kuanza kufanya shughuli mbalimbali za kilimo na baada ya kuambiwa kuwa ni maeneo ya uwekezaji kukawa na changamoto za wao kutoka” Amesema Sangu
Sangu amesisitiza kuwa wataweka mipaka ili wananchi walio ndani ya eneo la uwekezaji watambue na kufanya utaratibu wa kutoka ili wawekezaji wasipate ukakasi na wakabadili mawazo ya kufanya uwekezaji kufuatia migogoro inayoendelea na kupoteza fursa ya kuendeleza mkoa na nchi kwa ujumla.

Inaelezwa kuwa wananchi hao waliovunjiwa nyumba zao walijenga katika maeneo yaliyokwishalipiwa fidia na kwamba waliolipwa waliamua kuwatapeli kwa kuwauzia maeneo hayo. hata hivyo Mitaa hiyo ilihakikiwa na kupewa anuani za makazi na vibao vya mitaa kusimikwa.
Buha FM ilishuhudia vibao vyote viking’olewa siku chache kabla ya uvunjaji huo kufanyika na kuwaacha wananchi hao midomo wazi, mimea katika makazi hayo iliyotarajiwa kuzalisha mazao ya chakula hususani Mahindi imeharibiwa vibaya
Hata hivyo baadhi ya wananchi wakazi wa eneo lililovunjwa wameonesha ushahidi wa umiliki halali wa viwanja ikiwemo nakala za malipo ya urasmimishaji wa ardhi, vibali vya ujenzi kutoka ofisi ya mkurugenzi wa manspaa ya Kigoma-Ujijji na nyaraka nyingiine zinazowatambulisha
This Post Has 0 Comments