skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amefanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Kasulu, Kigoma Vijijini na Buhigwe mkoani Kigoma kwa lengo la kukagua mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III) ambapo pia aliwasha  umeme katika baadhi ya Vijiji.

Akiwa wilayani Kasulu, Dkt Kalemani alikagua kazi zinazofanywa na mkandarasi katika Kijiji cha Ruhita ambapo alikuta Kijiji hicho bado hakijaunganishwa umeme na kumuagiza Mkandarasi, kampuni ya CCCE Etern kufikisha umeme kijijini hapo baada ya siku 15.

Wananchi katika Kijiji cha Bulimanyi wilayani Buhigwe, Mkoa wa Kigoma wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati alipofika kijijini hapo kukagua miundombinu ya umeme.

Aidha, alimtaka Meneja wa TANESCO, Wilaya ya Kasulu kuhakikisha kuwa, anasimamia suala ya uchoraji wa ramani za kuingiza umeme ndani ya nyumba za wananchi kwani kuna baadhi ya watu binafsi wanaofanya kazi hizo wamekuwa wakiwatoza wananchi gharama kubwa bila kujali tofauti ya ukubwa au udogo wa kazi.

Vilevile, Dkt Kalemani alimtaka Meneja huyo kuhakikisha kuwa watu wanaofanya kazi za kufunga nyaya za umeme ndani ya nyumba za wananchi wanatambulika na TANESCO ili kuepusha utapeli na kufanya kazi chini ya viwango vinavyotakiwa.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Simon Anange alimweleza Dkt Kalemani kuwa, wananchi wa Kijiji hicho wamesubiri umeme kwa muda mrefu baada ya kupata ahadi ya kupelekewa nishati hiyo, hivyo wanaomba Mkandarasi akamilishe kazi hiyo mapema ili waweze kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo za kiuchumi.

Akizungumzia suala hilo, Dkt Kalemani alisema kuwa, Mkandarasi ambaye ni kampuni ya CCCE Etern ameanza kazi mwezi Januari mwaka huu tofauti na wanandarasi wa umeme katika maeneo mengine nchini ambao walianza kazi mwaka jana, hii ni kwa sababu ya masuala ya kisheria yaliyojitokeza hapo awali lakini sasa Mkandarasi huyo anaendelea na kazi.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Mpigo wilayani Kigoma Vijijini mkoa wa Kigoma kabla ya kuwasha umeme katika Kijiji hicho.

Akiwa wilayani Buhigwe, Dkt  Kalemani alikagua miundombinu ya umeme katika Kijiji cha Bulimanyi ambacho tayari kimeshafikishiwa  umeme na kaya zaidi ya Kumi zimeshaunganishwa na nishati hiyo na kumuagiza Mkandarasi kupeleka umeme katika Vijiji vyote vya Wilaya hiyo.

Dkt. Kalemani pia alikagua miundombinu ya umeme katika Kijiji cha Mkigo wilayani Kigoma Vijijini, ambapo pamoja na kuzungumza na wananchi, aliwasha umeme katika Kijiji hicho.

This Post Has 2 Comments

  1. Nimefurahishwa na taarifa ya kupelekwa umeme katika vijiji vya wilaya za Mkoa wa Kigoma.

    Umeme ni kiini cha maendeleo katika nchi yoyote duniani. Hivyo wananchi wa Kigoma vijijini watumie fursa hii kuvuta umeme kwa matumizi ya nyumbani, matumizi ya biashara kama vile kuchomelea, mashine za kukoboa na kusaga, mashine za kupukuchuka karanga na mahindi, mashine za kukamu mafuta ya alizeti na makarana, usindikaji vyakula, gereji, shughuli za ufugaji wa kisasa, n.k.

    Nimesikitika kuona ni nyumba kumi tu katika kijiji cha Bulimanyi ndo wameingiza umeme. Elimu zaidi itolewe juu ya umuhimu wa umeme na unavyopunguza gharama za mafuta ya taa n.k. Naamini Kasulu FM itakuwa chahchu kubwa ya kuhamasisha maendeleo katika Wilaya ya Kasulu na maeneo mengine ambako redio hii itasikika.

    Nashauri kuwe na picha na video nyingi zinazoonyesha matukio katika eneo husika zipambe habari.

    Picha zinaongea kuliko maneno.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma