skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Adela Madyane- Kigoma

WATOAJI wa huduma za bima nchini wametakiwa kuondoa hofu na kutafuta namna ya kuondoa changamoto ya kutohusisha vyombo vya usafiri wa majini hususan boti katika huduma ya bima ili waweze kukabiliana endapo majanga yatatokea.

Hayo yamebainika katika kikao cha pamoja baina ya wafanya biashara, wavuvi na wakala wa bima kilichoratibiwa na mamlaka ya bima nchini (TIRA) na kufanyika mkoani Kigoma kwa lengo la kutoa elimu ya namna ya kukabiliana na majanga yatokanayo na moto, ajali, mafuriko pamoja na matetemeko ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali la kutoa elimu hadi kufikia 80% kwa mwaka 2025 na wonanchi wote kuwa na bima ifikapo 2030.

Picha ya pamoja kati ya viongozi wa serikali, wakala wa Bima, wavuvi, wafabyabiashara,na mamlka ya wakala wa Bima katika ofisi za mkoa Kigoma

Wakijadili changamoto hiyo Shaban Yabulula mwenyekiti wa wakala wa forodha amesema kuna jumla ya boti 3700 zilizosajiliwa na shirika la uwakala wa meli (TASAC) na zote hazina bima hivyo ni jukumu la TIRA kushirikiana na mamlaka za usafirishaji majini kutafuta suluhu ya pamoja badala ya kujenga dhana kwamba boti zinazama, mbao zake kuoza na kwamba hazikidhi vigezo vya kuingia kwenye huduma za bima

“Mamlaka hizi zikutane kwaajili ya kufanya tathmini ya hatari, wajue kwa mwaka ajali ngapi za boti hutokea na kwasababu zipi kwakuwa eneo la forodha lina watu wengi na hawana uhakika na maisha yao” Amesema Yabulula

Naye mwenyekiti wa Wafanyakazi wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Abdul Mwilima amesema bandari ndogo ya Kibirizi husafirisha mizigo ya pesa nyingi takribani trilioni moja kuelekea nchi jirani ya Kongo kwa kutumia ujazo tofuati wa tani 50, 100 na 200 ila vyombo vinavyotumika kusafirisha mizigo havina bima kwakuwa vinaonekana si vyombo halali.

“Mji wa Kigoma ni mji wa bandari, kuna biashara zenye pesa nyingi, moja ya mazao ya ziwa Tanganyika ni uvuvi lakini wavuvi na vyombo vyao hawana bima, TIRA ichangamkie hii fursa na kujiingizia kipato kwani wanufaika ni wengi na wanahitaji bima” Amesisitiza Mwilima

Kwa upande wake meneja wa mamlaka ya bima kanda ya ziwa Sharif Ahmad amekiri uwepo wa changamoto hiyo na kwamba watakaa na watoa huduma ili kupanga mpango maalumu utakowezesha wavuvi na vyombo vyao kulindwa na bima kote nchini

“Ni agizo la serikali kwamba lazima vyombo vyote vya usafiri majini viwe na bima hivyo tutakaa na wavuvi na watoa huduma ya bima ili tuweze kupata fursa ya kutatua changamoto hizo na waanze kuulinda uchumi wao kuanzia ngazi ya familia na jamii kwa ujuma kwa kutumia bima” amesema Ahmad

Akizungumzia changamoto meneja huyo amesema kumekuwa na udanganyifu wa taarifa kutoka kwa wananchi na kuwaomba kuwa wakweli kwa kutoa taarifa sahihi.

Kwa upande wa watoa huduma Annastazia Ganja afisa wa benki ya NMB amesema wanao mpango wa kutoa elimu kwa wafanyaboashara wote ili kuhakikisha hata wafanyabiashra wadogo wanapata bima ili waweze kujikinga na majanga mbalimbali kwani bima ni mlinzi wa uchumi

“ Tunaendelea kufanya kampeni sehemu mbalimbali za biashara ikiwemo kwa wavuvi ili waweze kujua namna ya kujilinda na kulinda vitendea kazi vyao kwa kutumia bima ya wavuvi iliyipo kwenye taasisi yetu” amesema Ganja

Akizungumzia hilo Deogratius Sangu afisa biashara wa mkoa amesema kutatua changamoto ya bima kwa wavuvi na vyombo vyao yawapasa kuliweka jambo hilo kwenye baraza la biashara la mkoa litalofanyika baada ya maonyesho sabasaba na hata kwenye baraza la madiwani la mkoa ili kulipatia ufumbuzi mzuri.

“Ninatoa hamasa kwa jamii kutumia fursa iliyopo kwa kuweka kinga kama sehemu ya kulinda tulivyonavyo kwa kukata bima za vyombo, biashara na mali ili tuweze kuendelea na biashara hata majanga yakitokea” amesema Sangu

Vile vile Sangu ameitaka jamii kutumia bima kama sehemu ya ajira kwa kuchukua uwakala.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma