skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Adela Madyane – Kigoma

Afisa ustawi wa jamii wa manispaa ya Kigoma Ujiji Petro Mbwanji amewaomba wananchi mkoani humo kuwafichua walemavu waliofichwa ndani ili wapate mahitaji yao ya msingi ikiwemo haki ya kupata elimu.

Ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia na umuhimu wa afya ya uzazi kwa watu wenye ulemavu yaliyofanyika kwa udhamini wa shirikia la Norwegian Church Aid ( NCA) wakishirikiana na BAKAID.

“Wananchi wanaoficha watu wenye ulemavu wakiwemo watoto wanawanyima kupata haki zao za msingi, hivyo jamii tuachane na dhana potofu za kuwaficha na kuanza kuwatendea haki kwa kuwabainisha ili watambulike na wafanyiwe huduma zote za msingi kama binadamu wengine” Amesema Mbwanji

Kwa upande waJeremiah Mutagoma mjumbe wa kamati ya mkoa ya watu wenye mahitaji maalum amesema watu wanaoficha watu wenye ulemavu wanawafanyia ukatili wa kisaikolojia na kuzidi kudidimiza maendeleo yao hivyo wanapaswa kuwaweka wazi ili wapate mahitaji yao stahiki

Akizungumzia kuhusu afya ya uzazi ameiomba serikali kuweka miondombinu rafiki kwa wanawake wenye ulemavu hasa wakati wa kujifungua kwani vitanda vilivyopo maeneo mengi si rafiki kwao na inawafanya kujisikia vibaya kipindi cha kujifungua

“Serikali itusaidie kupata wataalamu wa lugha za alama kwenye maeneo muhimu ya huduma ikiwemo polisi na hospitali kwani watu wenye ulemavu wamekuwa wakipokea matibabu ya kimtazamo kutokana na changamoto ya kugha kati ya daktari na mgonjwa” ameeleza Mutagoma

Naye Adelina Jacob mlemavu wa ngozi kutoka manispaa ya Kigoma ujiji ameiomba serikali kuwawezesha njia rahisi ya upatatikanaji wa mafuta ya ngozi kwani baadhi yao huwapasa kukaa ndani kwa lengo la kujiepusha na mionzi ya jua inayowaathiri macho pamoja na ngozi zao

Kwa upande wake Juma Bawe afisa mradi kutoka BAKAID ameiomba jamii kutoa taarifa za baadhi ya watu wanaowaficha walemavu kwa lengo la kuweka mkakati maalumu ya kuwalinda dhidi ya matendo ya kikatili wanayofanyiwa ikiwemo kubakwa, na wengine kuuawa kwa dhana potofu za kishirikina

Ikubukwe mnamo mwezi Machi 6, mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan alisema bado kuna tatizo katika jamii ya baadhi ya wazazi kuwaficha watoto wenye ulemavu wakihisi kuwa na watoto hao ni laana huku akiwataka watu wenye ulemavu kujikubali walivyo.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma