skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mwandishi- Ofisi ya Waziri Mkuu.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendeleza kilimo cha mazao ya chakula na biashara ili kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika wa usalama wa chakula na ziada kuuza nje.
 
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 16, 2021) baada ya kukagua shamba la michikichi la kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) 821 KJ Bulombora akiwa katika ziara  ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Kigoma.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa licha ya kuwa mlezi wa mkoa wa Kigoma kisiasa amekuwa ni mdau mkuu wa kilimo cha Michikichi kama moja ya mazaoo makuu ya biashara mkoani Kigoma na dira yake ni kila kaya kuwa na shamba la zaoo hilo.

Waziri mkuu Kassim Majaliwa (aliyeinama) akikagua kitalu cha uzalishaji wa miche ya michikichi katika kambi ya Jeshi Bulombora mkoani Kigoma

Amesema Serikali inatekeleza dhamira hiyo kwa kufuatilia kwa ukaribu kilimo cha mazao hayo likiwemo na la michikichi kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa shamba hadi upatikanaji wa pembejeo. “Wazazi waanzishieni watoto wenu mashamba ya michikichi kwa ajili ya kuwakwamua kiuchumi ili wasiwe tegemezi.”
 
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi hususani waliopo kwenye mikoa inayolima michikichi washiriki katika kilimo cha zao hilo kwa ajili ya kukuza kipato chao na Taifa kwa ujumla. “Wekezeni katika kilimo cha michikichi kwa ajili ya maendeleo yenu pamoja na watoto wenu.”
 
Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali imeamua kulipa kipaumbele zao hilo ili kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini. Amesema Serikali inatumia zaidi ya sh. bilioni 400 kwa mwaka kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi, hivyo ufufuaji wa zao hilo utaliwezesha Taifa kuzalisha mafuta ya kutosha.

 Waziri Mkuu amewasisitiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Kigoma waratibu vizuri kilimo hicho ikiwa ni pamoja na kuwa na kanzidata itakayoonesha idadi ya wakulima, ukubwa wa mashamba yao na maeneo wanayolima ili kurahisisha utoaji wa huduma.
 
Amesema baada ya Serikali kupata mafanikio katika mazao ya biashara ya korosho, tumbaku, pamba, kahawa na chai, sasa imeamua kuongeza mazao mengine ya michikichi, mkonge, zabibu na parachichi ili nayo yaweze kuzalishwa kwa wingi na kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
 
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amelipongeza Jeshi la Kujenga Taifa na kambi yake ya Bulombora kwa kuitikia wito wa kulima zao la michikichi kwa vitendo na kwamba shamba hilo linatarajiwa kuwa la mfano kwa kilimo cha zao hilo.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma