skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mwandishi ofisi ya Waziri Mkuu na Anita Balingilaki – Buha FM, Simiyu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua mradi wa maji wa Ngulyati – Nyamswa wilayani Bariadi, mkoani Simiyu wenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 na kukabidhi mtambo wa kuchimba visima virefu vijijini ambao ni sehemu ya fedha za miradi ya UVIKO-19.

Akizungumza na wakazi wa Ngulyati mara baada ya kuzindua mradi huo leo (Jumamosi, Machi 25, 2023) Waziri Mkuu amesema mradi uliozinduliwa leo ni mojawapo ya malengo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaondolea wananchi adha ya kukosa maji.

“Tangu akiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alianzisha kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani. Rais wetu ameendelea kutoa fedha nyingi za miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi hawapati shida ya maji.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akitazama  mitambo ya kuchimba visima virefu vya maji baada ya kukagua na kuzindua mradi wa Maji wa Ngulyati- Nyamuswa wilayani Bariadi akiwa katika ziara ya Mkoa wa Simiyu, Machi 25, 2023. Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed na wa tatu kulia ni Naibu Waziri  Ofisi ya Rais Tamisemi, Dkt. Festo Dugange (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Ili kutekeleza agizo hilo, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa chombo cha watoa huduma ngazi ya jamii (GAISANGU) wasimamie maji hayo kwenye vilula (viosk) na kuhakikisha yanatoka saa zote bila mgao kwani tenki limejengwa kilimani ili kuwepo na mtiririko wa kutosha.

Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais ametoa magari yenye mitambo ya kuchimba visima ili yatumike kuchimba visima hivyo kwenye maeneo ya vijijini ambako kuna vyanzo vya maji na kwamba walioko mkoani wasiyazuie magari hayo kufanya kazi vijijini.

Akitoa mfano, Waziri Mkuu amesema: “Kuna mkoa nilienda nikakuta kuna mvutano baina ya RUWASA mkoani na wilayani. Wilayani wanaomba gari likachimbe visima vijijini, wao wa mkoani wanazuia hadi wapewe malipo. Sitaki kuona huo mvutano hapa Simiyu, kikubwa mhakikishe magari yana mafuta, mambo ya malipo mtamalizana baadaye.”

Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Ngulyati akiwemo Leah Bulenge na Ester Mboje  wameishukuru serikali kwa kutekeleza mradi huo wa maji katika maeneo yao wakikiri kuwa maji lilikuwa ni tatizzo katika jamii yao. tazama video ya wananchi hapa chini

Leah Bulenge na Ester Mboje  wameishukuru serikali

Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa RUWASA, Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mariam Majala alisema mradi utatoa huduma kwa wananchi 10,106 wa vijiji vya Ngulyati, Nyamswa na Nyasosi na kwamba mahitaji ya maji katika vijiji hivyo vitatu ni lita 271, 900.

Mradi huo ulioanza kujengwa Mei, 2022 na kukamilika Januari, 2023 umeanza kutoa huduma na una uwezo wa kuzalisha maji lita 15,800 kwa saa sawa na kupampu lita 284,000 kwa saa 18 kwa siku.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipozindua mradi wa Maji wa Ngulyati – Nyamuswa wilayani Bariadi akiwa katika ziara ya Mkoa wa Simiyu, Machi 25, 2023. Wengine kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya  Rawanda, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mariam Majala na kulia ni Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mbunge wa Bariadi, Mhandisi Kunde Mathew.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Kabla ya kwenda Ngulyati, Waziri Mkuu alizindua tawi la NBC wilayani Bariadi ambalo ni la kwanza katika mkoa wa Simiyu.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma