skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mwandishi wetu, Lindi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekabidhi pikipiki 100 zenye thamani ya sh. milioni 260 kwa vijana wa wilaya ya Ruangwa ili wazitumie kufanya biashara ya usafirishaji wa abiria na miziko na kujiongezea kipato ili kukabiliana na tatizo la umasikini na ukosefu wa ajira.

Akizungumza na vijana wa Ruangwa kwenye hafla ya kukabidhi pikipiki hizo iliyofanyika mwishoni mwa wiki, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, Waziri Mkuu alisema utoaji wa pikipiki hizo ni muendelezo wa mpango wa ofisi ya Mbunge wa kuwawezesha vijana, wanaume, wanawake na wazee.

Mwaka 2016/2017 tulichukua pikipiki 235 na kuzigawa kwenye wilaya yote hii. Na jambo zuri kwa sasa, kwenye Serikali ya awamu ya sita, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Tanzania na yeye ameamua kuwa na kada ya wasafirishaji wa wadogo, wa kati na wakubwa.”

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa  Ruangwa aliwaeleza vijana hao watambue kwamba na wao ni wasafirishaji wa usafiri wa kawaida kwa kutumia pikipiki.

Waziri Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Kassim Majaliwa  akizungumza na baadhi ya vijana wa wilaya ya Ruangwa baada ya kukabidhi pikipiki 100 zenye thamani ya shilingi milioni 250 kwa ajili ya kufanya biashara ya usafirishaji,  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Mapema, akielezea mradi huo, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo wa soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, Bw. Martin Mbwana alimweleza Waziri Mkuu kwamba pikipiki hizo zitakopeshwa kwa bei ya sh. milioni 2.6 bila riba yoyote na kwamba muda wa marejesho ni miezi nane.

“Kuanzia sasa hadi Desemba, mwaka huu mtu anapaswa awe amekamilisha mkopo wake. Na kianzio ni kati ya sh. 500,000 hadi 700,000. Mkopo huu umetolewa chini ya mdhamini mkuu, Bw. Mpaluka Hashim Mtopela,” alisema.

Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango ya biashara na kuongeza: “Nikiwa mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo wa soko la Kariakoo, niko hapa Ruangwa ili kuwawezesha vijana wa Ruangwa,” alisema.

Kwa upande wake, mdhamini mkuu wa pikipiki hizo, Bw. Mpaluka Hashim Mtopela alimshuruku Waziri Mkuu kwa kuamua kuwajali vijana wa jimbo lake.

Mwaka 2016 ulitoa pikipiki 235 ambazo zimewezesha vijana zaidi ya 600 kuishi maisha mazuri wao na familia zao. Wako waliopewa pikipiki moja lakini leo hii wanamiliki pikipiki tatu hadi nne.” alisema Bw. Mtopela

“Hii ina maana leo tukimpa kijana sh. milioni 2.6, baada ya muda ataweza kutengeneza shilingi milioni 7. Vijana hawa nimewachukulia dhamana kwa sababu ninaamini wanaweza kuzirejesha. Safari hii tumechukua pikipiki lakini muda ujao tutachukua mashine ya kufyatulia matofali au ya kumwagilia bustani kwa sababu tunao vijana wenye uwezo,” aliongeza Mtopela.

Mradi kama huu wa kusaidia vijana kiuchumi kupitia utoaji wa pikipiki za kusafirishia abiria maarufu bodaboda umefanyika bia katika Jimbo la Kasulu mjini mkoani Kigoma kupitia kwa Mbunge wake Profesa Joyce Ndalichako ambaye pia ni waziri katika ofisi ya waziri mkuu, Kazi, Vijana na wenye Ulemavu.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma