skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mwandishi wetu, Urusi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo (Jumapili, Julai 30, 2023) alikuwa miongoni mwa Wakuu wa Nchi na Serikali waliohudhuria Maonesho ya Gwaride Maalum la Jeshi la Wanamaji la Urusi yaliyofanyika Senatskaya Marina, St. Petersburg, Urusi.

Viongozi hao ni wale walioshiriki Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi jijini St. Petersburg, Urusi ambako yeye alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Rais wa Urusi, Vladimir Putin wakati alipohudhuri  gwaride la Jeshi la Wanamaji la nchi hiyo lililofanyika St. Petersburg nchini Urusi, Julai 30, 2023. Kushoto ni mkewe Mama Mary Majaliwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Maonesho hayo yamefanyika ikiwa ni siku ya Jeshi la Wanamaji la Urusi na maadhimisho  ya kukumbuka kuanzishwa kwa jeshi hilo ambayo hufanyika Julai 30, kila mwaka.

Moja kati ya madaraja mengi yanayofunguka likiwa limefunguliwa kuruhusu msafara wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin kupita wakati wa gwaridei la jeshi la Wanamaji la nchi hiyo lililofanyika St. Petersburg nchini Urusi, Julai 30, 2023.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Katika maonesho hayo Rais wa Urusi, Vladmir Putin alipita kwenye boti maalum akiwasalimia wananchi waliojipanga kwenye kingo za mto Bolshaya Neva na kupokea salamu za kijeshi. Alipomaliza akavushwa na boti ndogo kwenda kwenye jukwaa maluum na kuhutubia Taifa.

Baada ya hapo meli na boti za kivita zilipita mbele ya jukwaa kuu na kutoa heshima. Kisha akaenda kuwasalimia mmoja baada ya mwingine viongozi wa Afrika waliohudhuria maonesho hayo na baadaye alipanda nao kwenye boti hiyo maalum.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma