skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mwandishi wetu, Kasulu

Moja ya mambo ambayo hadi sasa yanaleta utata kwa wazee ni pamoja na haki ya kupata matibabu bure na yasiyo na bughudha, hata hivyo licha ya mikakati mbalimbali kuwekwa na serikali pamoja na asasi za kiraia kuhusu kuwapa haki ya afya na mahitaji mengine, wazee bado wanakabiliwa na mbinyo wa kisera na kisheria pamoja na mitazamo hasii ya jamii.

Tafiti zinabainisha kuwa changamoto za kiafya ndiyo kiini cha unyonge wa wazee wengi hususani wastaafu wa serikali ambao wanaamini kuwa wana haki ya kuhudumiwa kutokana na mchango waoo kwa serikali na taifa. Asilimia 80 ya wazee wanakumbana na vikwazoo vingi vya matibabu katika zahanati na vituo vya afya na hivyo kulazimika kwenda katika hospitali kubwa au za rufaa bila kufuata mlolongo wa taratibu za kupata rufaa, na wengi hukosa matibabu stahiki.

Kutokana na hali hiyo, wazee wengi hupoteza matumaini na kupoteza maisha kutokana na msongo wa mawazo yanayotokana na kile kinachotajwa kuwa ni ubaguzi wa kijamii na kutelekezwa na watoto au ndugu wengine.

Baadhi ya wazee wanaoishi katika mazingira magumu wilayani Kasulu mkoani Kigoma

Kwa mujibu wa sera ya Wazee Tanzania, uzee ni hali ya kuwa na umri mkubwa unaoanzia miaka sitini na kuendelea. Wazee wako katika makundi makuu mawili ya wastaafu wa Utumishi wa Umma serikalini na katika mashirika mbalimbali pamoja na wazee waliokuwa wamejiajjiri wenyewe katika shughuli za kijamii hususani Kilimo

Hali hii nimelivutia shirika la Endeleza Wazee Kigoma, kuanzisha mpango mahususi wa kujenga kituo cha wazee ili kitumike kama chachu ya kudai haki na kupata huduma mbalimbali.

Mwalimu Mstaafu Clotilda Kokupima mkurugenzii wa shirika la Endeleza Wazee Kigoma

Kwa mujibu wa Mwalimu mstaafu Clotrida Kokupima ambaye ni mwasisi na kiongozi wa shirika la wazee Kigoma na mwenyekiti wa mtandao wa mashirika ya kutetea haki za wazee Tanzania, Malalamiko ya kijamii na kisera ni mengi, lakini ni kwa namna gani wazee Tanzania hususani Kigoma wanavyohangaika na kukosa huduma, na pia tunahoji ni kwa namna gani serikali na wadau wa maendeleo wanavyoshughulikia malalamiko na madai ya wazee?

Shirika la Endeleza Wazee Kigoma (EWAKI) limebuni mradi mahususi wa kituo cha Furaha kwa ajili ya kuwafuta machozi wazee mkoani humo hususani wanaoishi katika mazingira magumu, wasio na walezi, wagonjwa na wazee wanataaluma.

Chini ya mradi huo uliopewa jina la kituo cha Burudani kwa wazee (recreation centre) zaidi ya wazee 64 kutoka wilaya zote za mkoa wa Kigoma ambao hawana makazi maalumu watapatiwa hifadhi na kupata matunzo mbalimbali ikiwemo huduma za afya.

Akizungumza na Buha FM, Mwasisi wa shirikila la EWAKI Mwl. Clotrida Kokupima mwenye umri wa miaka 87 amebainisha kuwa uanzishwaji wa kituo hicho umetokana na tafiti zilizofanywa na EWAKI kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali na wahisani kubaini kuwepo kwa kundi kubwa la wazee ambao wamekosa matumaini na wanaishai katika maisha hatarishi.

Tumefanya utafiti mkoa mzima na kubaini kuwa wapo watu ambao hadi sasa hawatambuii wazee wala kuthamini mchango wao kwa kaya, jamii na taifa wakati wa ujana wao, jamii imejisahau na hata baadhi ya viongozi wa serikali hawaamini kuwa nao ni wazee watarajiwa na kwa sababu hiyo wanapuuza madai na mahitaji ya wazee na kupelekea wengi wao kuishi katika maisha magumu sana.” Alisisitiza Kokupima.

Kituo cha Wazee Kasulu kinachojengwa katika Mtaa wa Nyumbigwa Mjini Kasulu, kitahudumia wazee zaidi ya 64 katika awamu ya kwanza.

Mwl Mstaafu Kokupima amebainisha kuwa kituo hicho kitakachogharimu zaidi ya sh. 500 milioni kitakuwa ni sehemu ya kurejesha furaha kwa wazee, kutoa huduma mbalimbali za unasishi na matibabu, kituo cha mazoezi ya viungo, pamoja na mradi wa ujasiriamali kwa wazee ambao bado wana nguvu za kufanya kazi ili wajiendeleza na kupata kipato cha ziada.

Hata hivyo ameeleza kukabiliwa na changamoto kubwa ya kukosa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo utakaokuwa na majengo maalumu 6, na kwamba hadi sasa tayari jengo moja la utawala limekamilika na majengo mengine yatajengwa baada ya kupata wahisani.

Baadhi ya mashirika ambayo yamejitokeza kuunga mkono mradi huo ni pamoja na Segal Family Foundation, UNICEF Tzanzania pamoja na Help Age international ambao wameonesha kuguswa na changamoto za wazee nchini Tanzania.

Video inayoelezea kuhusu shirika la EWAKI historia na majukumu yake kwa wazee

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, changamoto kubwa inayowakabili wazee nchini Tanzania ni kukosa matibabu ya uhakika, kukosa wataalamu wa kutosha wa afya na magonjwa ya wazee, urasimu katika vituo vya kutoa huhuma za afya, kukosa Bima ya afya ya wazee, kutengwa na kaya au kutelekezwa na watoto au ndugu, kupata pensheni ndogo, hujuma za kifedha kwa wazee na kukosa makazi kwa wazee ambao hawakuwa watumishi wa umma.

Kufuatia hali hiyo shirika la Endeleza Wazee Kigoma (EWAKI) linatoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kuunga mkono juhudi za kumkomboa mzee wa Kigoma kwa kuchangia ujenzi wa kituo cha wazee pamoja na huduma nyingine za kijamii ikiwemo masuala ya msaada wa kisheria.

Mkoa wa Kigoma unakadiriwa kuwa na wazee wapatao laki moja wengi wao wakiishi katika mazingira magumu yanayohitaji usaidizi.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma