skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania imetoa boti ya kisasa yenye thamani ya shilingi milioni 32 na laki 9  kwa maafisa uvuvi wilayani Muleba mkoani Kagera ili kuendeleza doria  katika kudhibiti uvuvi  haramu  katika ziwa Viktoria.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa boti hiyo uliyofanyika  katika mwaro wa katembe Magarini  wilayani Muleba  kwa niaba ya Serikali mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge ametoa maelekezo kwa maafisa uvuvi wilayani humo kutumia boti hiyo kwa manufaa makubwa ya wananchi na malengo yaliyokusudiwa na Serikali ili kufanikisha kulinda rasilimali zote zilizomo ndani ya ziwa viktoria  hasa eneo la visiwa vilivyopo wilayani Muleba hali itakayokuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge akitoa maelekezo kuhusu udhibiti wa uvuvi haramu mkoani humo

RC Mbunge amewaeleza wananchi wilayani Muleba kuwa boti hiyo iliyopelekwa imetokana na nguvu zao wenyewe wana Muleba kwa kuwa yamekusanywa mapato yanayolipwa na wananchi kwa  kushirikiana  na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka nje lengo likiwa ni kuendelea kuwahudumia wananchi wa maeneo hayo ikiwemo kutoa ulinzi uliyo bora ndani ya ziwa Viktoria.

“Serikali ya mhe.Rais  Mama Samia Suluhu Hassani kupitia wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutambua umuhimu kwa suala la kutunza bidhaa adimu ambao ni Samaki waliopo kwenye ziwa letu kwa kuleta boti ili iwezekuwa na ulizi sahihi ili vizazi vijavyo viwezekuja kukutana na mazalia ya Samaki yatakayokuwepo”.Alisema RC Mbunge

Naye Afisa Uvuvi kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi hapa  nchini  Bw. Masanja Kadashi  amesema kuwa kipindi cha hapo nyuma suala la Uvuvi haramu lilikuwa limeshamiri kwa kiasi kikubwa na kuibua changamoto ikiwemo kukosekana kwa vitendea kazi katika kukabiliana na uvuvi haramu na kusema kuwa ujio wa chombo hicho itawarahisishia kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa wakati wote.

“Tunapokuwa na vyombo kama hivi kuna suala la utoroshaji wa mizigo watu wanapita maji ya juu kwa ajili ya kusafirisha mazao yetu kupeleka nchi ya Uganda pia katika suala la uokoaji watu wakizama inakuwa ni rahisi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wepesi kwa wananchi wetu na kingine kwa ajili ya Ulinzi wa usalama wao wawapo majini”.Alisema Kadashi

Katika kuhakikisha rasilimali zilizomo katika ziwa Viktoiria zinawanufaisha wananchi kwa upande wao baadhi ya wakaazi wa  mwaro wa Katembe Magarini wilayani Muleba mkoani Kagera wameishukuru Serikali yao kwa kutoa boti kwa eneo hilo ambapo wamesema kuwa  ujio wa chombo hicho utasaidia kuendelea kudhibiti utoroshaji wa mazao ya Samaki na Dagaa ikiwemo kukomesha  uvuvi  unaoendeshwa na baadhi ya wavuvi pasipo kufuata sheria zilizowekwa na mamlaka husika za Serikali ya Tanzania .

Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Mei mwaka wa 2020, Serikali ya mkoa wa Kagera kaskazini magharibi mwa Tanzania ilizindua Boti tatu za doria katika wilaya ya Muleba zilizokuwa na thamani ya shilingi milioni 173 kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kukabili upotevu wa mapato yatokanayo na shughuli ya Uvuvi katika ziwa Viktoria.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma