skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesisitiza uwajibikaji kwa kila mtumishi wa Wakala ili kutekeleza jukumu lake kuu la kuhakikisha wananchi waishio vijijini wanatumia nishati bora kama zinazotumika mijini.

Alikuwa akizungumza katika kikao kazi cha wafanyakazi wa REA kilichofanyika Septemba 11, 2023 jijini Dodoma kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuboresha utendaji kazi.

“Kila mmoja wetu anapaswa kuwa na utashi, kuweka jitihada na maarifa ili matunda ya kazi yetu yaonekane kwa wananchi,” amesisitiza.

Akieleza zaidi, Mhandisi Saidy amesema wafanyakazi wa REA wanapaswa kuhakikisha utendaji kazi wao unaakisi dhamira ya Serikali ya kuwapatia fursa wananchi waishio vijijini kutumia nishati bora sawa na wale wanaoishi mijini.

Amesema kuwa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala inaendelea vizuri na akawataka wafanyakazi kuendelea na moyo wa utendaji kazi kwa bidii ili miradi mipya iliyoanza kutekelezwa ikamilike kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), Tawi la REA, Swalehe Kibwana aliushukuru Uongozi wa Wakala kwa kujenga utaratibu wa kuzungumza na wafanyakazi ili kuwapatia fursa ya kueleza changamoto ikiwa zipo na kutoa maoni yao kuhusu masuala mbalimbali ya kazi.

Katika kikao hicho, wafanyakazi mbalimbali walitoa maoni kuhusu maeneo ya utendaji kazi yanayopaswa kuboreshwa na ni kwa namna gani.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma