skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Yumo anayetuhumiwa kwa makosa ya Kulawiti

Na Anita Balingilaki,Simiyu

Jeshi la polisi mkoa wa Simiyu limewakamata watuhumiwa 37 wa makosa mbalimbali yakiwemo ya wizi, kupatikana na nyara za serikali sambamba na ulawiti.

Hayo yamesemwa na kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu ACP Edith Swebe wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa katika kipindi cha Mei 25 hadi Juni 22 mwaka huu.

Aidha kamanda Swebe amesema kwa kushirikiana na ofisi ya taifa ya mashtaka wamewafikisha watuhumiwa mahakamani na hukumu za kesi zimetolewa.

Miongoni mwa waliohukumiwa ni pamoja na John Anthony (21) Mkazi wa Nanga wilayani Itilima ambaye amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kumuingilia kinyume na maumbile mtoto mwenye umri wa miaka 13 mwanafunzi wa shule ya msingi Nanga.

Mwingine aliyehukumiwa ni Japhet Amos (24) mkazi wa Meatu ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka thelathini kwa kosa la kubaka na kumpatia mimba mwanafunzi.

“Kupatikana na nyara za serikali mtuhumiwa Hussein Masanja (42) mkazi wa Mawangundo amehukumiwa kwenda jela miaka thelathini,kupatikana na bangi mtuhumiwa Joyce Mwita (23) mkazi wa katoro Geita amehukumiwa kifungo cha miaka thelathini jela” amesema kamanda ACP Swebe.

Katika hatua nyingine kamanda Swebe amesema kupitia operesheni iliyofanywa na jeshi hilo kwa kushirikiana na shirika la umeme nchini (TANESCO) mkoani hapo, wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili wanaojihusisha na biashara ya vyuma chakavu wakiwa na nyaya za copper kg 53 ambapo nyaya hizo zilitokana na uharibifu na wizi wa miundombinu ya shirika la umeme.

Kamanda Swebe amesema wizi wa nyaya hizo umelisababishia shirika la umeme mkoani hapo hasara ya shilingi milioni ishirini na moja laki mbili na elfu arobaini ( 21,240,000) na kitendo hicho kimesababisha ukosefu wa huduma ya umeme kwa vijiji vya kasoli na kilalo vilivyopo wilayani Bariadi mkoani Simiyu.

Aidha watuhumiwa wengine sita walikamatwa kitongoji cha Itongo wilayani Busega wakiwa na vifaa vya kuvunjia milango na madirisha ambavyo ni mkasi mkubwa mmoja,mkasi mdogo mmoja,praizi ndogo moja na kipisi cha nondo.

Jeshi la polisi mkoa wa Simiyu limetoa onto kali kwa wananchi wanaojihusisha na matendo ya uhalifu kuacha mara moja kwani hatua kali zitaendelea kuchukuliwa dhidi yao.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma