skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Adela Madyane, Kigoma

Jumla ya watoto 1675 wenye umri chini ya miaka mitano katika halamashauri ya wilaya ya Kigoma wamechanjwa chanjo ya surua katika kampeni ya chanjo ya UVIKO 19 pamoja na chanjo za kawaida za watoto baada ya kutochanjwa katika utaratibu wa kawaida

Kampeni hiyo iliyofanyika katika vituo vya afya 26 vya halmashauri hiyo, inatekelezwa na Taasisi ya Benjamini Mkapa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Benki ya dunia katika kata ya Mahembe yenye vijiji vinne ambavyo ni Chankambwimba, Mahembe,  Mahembe kati pamoja na Kabanga kwa kipindi cha siku sita kuanzia Machi11-16, 2023. 

Akizungumza katika kilele cha kampeni hiyo mratibu wa chanjo wa halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Yusuph Zuila amesema kati ya watoto 1675 waliochanjwa 626 wamechanjwa kwa mara ya kwanza na 1049 kwa mara ya pili na kwa upande wa UVIKO 19 watu 7377 sawa na asilimia 104 .2 wamechanjwa jambo lililovuka matarajio yao ya awali ya kufikia watu 7082.

Zuila ameisisita jamii ya Kigoma kujiepusha na kuacha imani potofu na maneno ya uchochezi yenye kuleta taharuki na kusababisha baadhi ya wazazi kuacha kuwapeleka watoto kuchanjwa jambo ambalo limekuwa ni changamoto katika uhamasishaji kwa kipindi chote cha kampeni na kuwaomba wazazi kuwapeleka watoto wao kliniki kwaajili ya kupata chanjo kwa muda uliopangiwa na mtoa huduma.

“Nawasisitiza viongozi wa kata, vijiji,vitongoji na viongozi wa dini kukemea vikali imani potofu na maneno ya uchochezi juu ya huduma za chanjo na kusababisha baadhi ya wazazi kuzuia watoto wao wasipate chanjo, hakikisheni mnatoa elimu sahihi kama inavyoelekezwa na watoa huduma na kuwapatia ushirikiano unapohitajika kwani chanjo ni zile zile zinazotolewa siku zote ambazo mimi na wewe tulichanja” Amesema Mratibu wa chanjo.

Mtoto akipatiwa chanjo katika kijiji cha Mahembe wilaya ya Kigoma nchini Tanzania

Naye kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Jabil Timbako, amesema kampeni hiyo imesaidia kuwaainisha, kuwafuatilia na kuwachanja watoto walioasi chanjo na kusisitiza kuwa endapo watoto watachanjwa kwa ratiba na  mahudhurio yaliyopangwa kliniki itasaidia kuwakinga watoto na magonjwa mbalimbali kwakuwa kinga mwili zao zitaimarika.

Kwa upande wa kaimu meneja mradi kutoka taasisi ya Benjamin Mkapa Zawadi Dakika amezitaja mbinu mbalimbali zilitotumika katika kufanikisha kampeni hiyo kuwa ni pamoja na kuwafuata watu majumbani mwao pamoja na mashambani ambapo alizishukuru  timu za uendeshaji wa huduma za afya mkoa na wilaya (RHMT na CHMT), wahudumu wa afya ngazi ya Kituo cha afya,  ngazi ya Jamii (CHW) na viongozi wa vijiji kwa kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo.

Amesema lengo la kampeni hiyo ni kutoa chanjo ili kujikinga na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ikiwemo ugonjwa wa UVIKO 19, magonjwa ya Surua, Kupooza kwa Ghafla (Polio), Kifua Kikuu (TB), Pepopunda, Dondakoo,Kifaduro,Homa ya Ini, Kuhara na Saratani ya Mlango wa kizazi.

Akizungumza kwa niaba ya baadhi ya wazazi ambao watoto wao wamechanjwa Rehema Kigezi mkazi wa kijiji cha Mahembe amesema bado huduma ya chanjo haieleweki vizuri kwa wananchi huku wengi wao wakiwa na imani potofu kwakuwa wengi hawajui nini maana ya chanjo na kuziomba mamalaka husika kuendelea kutoa elimu na mafunzo mbalimbali juu ya umuhimu wa chanjo ili wazazi wengi waweze kujitokeza na kuwapatia huduma ya chanjo watoto wao.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma