WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua jengo la wagonjwa wa dharura kwenye hospitali ya wilaya ya…
Mwandishi na Joel Daud, Muleba
Watu Ishirini na sita 26 wanaosadikiwa kuwa ni wafanyabiashara haramu wa kahawa wamekamatwa na vyombo vya usalama wilayani Muleba mkoani Kagera wakisafirisha zao hilo kinyume na utaratibu wa sheria uliowekwa na Serikali wa kuuza kwenye minada inayotambulika kupitia vyama vya msingi.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Muleba Bw.Toba Nguvila wakati wa opereshani iliyofanywa na vyombo vya ulinzi wilayani humo na kufanikiwa kukamatwa kwa wafanyabiashara hao waliokuwa wakisafirisha kahawa zaidi ya kilogramu elfu 35 na kukamata magari 25 yaliyokuwa yakitumika kusafirisha kahawa hiyo

Katika tukio hilo Bw.Nguvila amesema watu hao walikamatwa wakipeleka maeneo yasiyokuwa rasmi kwa zao la kahawa, hali iliyotafsiriwa kuwa ni utoroshaji zao hilo na kulipeleka kusikojulikana jambo linaloikosesha serikali mapato na kuwapunja wakulima
“Kimsingi kitakwimu serikali inawezakukosa takwimu halisi za uzalishaji mimi kama mkuu wa wilaya na wenzangu tutaendelea kuwafundisha wananchi wetu wawezekujua vizuri utaratibu huu mpya wa mnada wa kahawa ambao kimsingi una tija na ufanisi mkubwa sana kwa wakulima wetu katika kuondokana na umaskini”.Alisema
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya Bw.Tova Nguvila aliwataka wananchi wilayani humo hasa wakulima wa zao la kahawa kuacha mara moja tabia ya kuuza zao hilo kwa mfumo usio rasmi kwa kuwa hawatanufaika badala yake wafuate utaratibu mzuri uliyowekwa na serikali ili kuwainua wakulima wake.
“Inawezekana mwaka huu wengine walizoea utaratibu ule wa zamani na mimi nasema kama kuna mfanyabiashara yeyote kwenye wilaya yetu hii ya Muleba aliyewekeza fedha kwa mkulima ili auziwe kwa bei anayotaka yeye, atanisamehe sana watanisamehe kwa sababu mkulima kahawa zake zitakwenda chama cha msingi baada ya kuuza ile kahawa fedha yake atarudishiwa aliyoweza kwa mkulima”. Alisema DC Nguvila.
Naye mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba Bw. Elias Kayandabila alisema kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi juni mwaka huu wa 2022 wilaya ya Muleba imefanikiwa kuendesha minada sita kwa utaratibu uliowekwa na bodi ya kahawa ambayo minada hiyo ilifanyika Bukoba mjini.
“Hadi sasa kahawa ambayo inakadiriwa kutoka kwetu kwa kipindi hiki kifupi kwa msimu inakaribia kilogramu laki mbili na elfu thelasini na nne na miatisa ishirini na tatu za kahawa. Kwa mwaka jana wa 2021 kabla ya utaratibu huu wa minada kwa kahawa aina ya Robusta ya maganda mkulima alipata Tsh.1,200 kwa kg 1 ikilinganishwa na mwaka huu inauzwa kwa Tsh.1650 hadi 1760 kwa kg 1”.Alisema Kayandabila
Kwa upande wao baadhi ya wananchi na wakulima wa zao la kahawa wilaya ya Muleba mkoani Kagera waliiomba serikali kupitia Idara pamoja na mamlaka za utawala ndani ya Halmashauri hiyo kupeleka elimu ya kutosha kwa wakulima wa kahawa ili watambua nia ya serikali yao ya kutaka kuwaondoa kwenye unyonyaji unaofanywa na walanguzi wadogo wadogo wa zao hilo maarufu kama Butura na badala yake wauze kahawa zao kwenye minada inayotambuliwa na serikali ili wapate kunufaika zaidi.