skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki, Simiyu

Unyonyeshaji wa maziwa ya mama unatajwa kuwa miongoni mwa haki ya msingi ya mtoto ambayo inapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kutekelezwa kikamilifu na huchangia kuboresha lishe bora na uhakika wa chakula kwa mtoto katika hali ya kawaida na hali ya dharura.

Unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni afua muhimu inayosaidia kuimarisha afya ya mtoto mchanga na mdogo kwa kumkinga na maradhi ya kifua, kuharisha na ngozi na hivyo  kumfanya mtoto akue kwa kuendana na uzito sawia na umri wake na kumuepusha  na athari za ukondefu, uzito pungufu na  udumavu.

Afisa lishe mkoa wa Simiyu Dkt Chacha Magige  anasema unyonyeshaji wa maziwa ya mama kikamilifu humuepusha mtoto kupata uzito uliokithiri kulinganisha na umri wake, ambapo mtoto akiwa na uzito uliokithiri huwapelekea kupatwa na magonjwa yasiokuwa ya kuambukiza  hawapo mtu mzima.

Dkt Magige anasema afua ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama hutekelezwa na kupimwa na viashiria mbalimbali  ikiwemo uanzishwaji wa maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa mtoto na afua hii hukinga ubongo wa mtoto kupatwa na upungufu wa sukari hali inayoweza kusababisha mtoto kupatwa na degedege na kubabisha matitizo ya ubongo.

” kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama pekee hadi kukamilisha umri wa miezi sita bila chakula kingine afua hii humuepusha mtoto kupatiwa vyakula ambavyo mfumo wake wa umeng’enyaji hauwezi kutekeleza kikamilifu hali hii huweza kuvuruga mfumo mzima wa umeng’enyaji na ufyonzaji wa virutubishi na kupelekea maradhi mbalimbali ya muda mrefu ikiwemo mzio (Allergy), shinikizo la damu (Pressure), vidonda vya tumbo na matatizo ya figo…unyonyeshaji mtoto sambamba na kumpatia chakula cha nyongeza afua hii humsaidia mtoto kupata virutubishi vya nyongeza kutokana na vyakula huku akiendelea kunyonya maziwa ya mama”anasema Dkt Magige.

Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa za mwaka 2019 kutoka Tanzania National  Nutrition Survey  (TNNS) zinaonesha asilimia 92.2 ya wanawake wanachagua kuwanyonyesha watoto wao, asilimia 62.0 ya watoto huanzishiwa kunyonya maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa, asilimia 55.7 ya watoto wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee ndani ya miezi sita ya mwanzo, watoto wanaoendelea kunyonyeshwa hadi kufikia umri wa mwaka mmoja ni asilimia 93.0 na watoto wanaoendelea kunyonyeshwa hadi kufikia miaka miwili ni asilimia 43.2.

Aidha kwa mujibu wa TNNS asilimia ya watoto wanaoanzishiwa vyakula vya nyongeza katika umri sahihi wa miezi sita ni 73.3, asilimia 53.2 ya watoto hupatiwa mlo kamili wenye mchanganyiko sahihi wa makundi matano ya vyakula, asilimia 35.9 ya watoto wenye umri wa miezi 6 hadi 23 wanapewa idadi sahihi ya milo kwa siku kulingana na umri wao na asilimia 45.8 ya watoto wenye umri wa miezi 6 hadi  23 wanapewa milo yenye ubora wa kukidhi mahitaji ya  kilishe ya watoto.

Dkt Magige anasema kwa mkoa wa Simiyu mwenendo wa uanzishwaji wa maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa kwa watoto wachanga kwa mwaka 2019 ni asilimia 94.8 , mwaka 2000 ni asilimia 93.9, mwaka 2021 ni asilimia 93  na kwa mwaka 2022 ni asilimia 95.4 huku mwenendo wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita watoto wachanga na wadogo  kwa mwaka 2019 ni asilimia 218, mwaka 2000 ni asiimia 204, mwaka 2021 ni asilimia 140 na mwaka 2022 ni asilimia 96.

Kuhusu muongozo wa wizara ya afya, kuhusu unyonyeshaji unapendekeza  watoto wenye umri wa miezi 0 hadi 23 waanze kunyonya maziwa ya mama mara tu baada ya kuzaliwa katika kipindi kisichozidi saa moja baada ya mama kujifungua, wapewe maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa na hii inamaanisha  hawapaswi kupewa maji, juisi, chai, mchuzi au vyakula vingine vyovyote na katika kipindi hicho  wanaweza kupewa dawa au kitu kingine chochote iwapo tu itashauriwa na mtaalamu wa afya.

Dkt Magige anasema muongozo wa wizara hiyo unataka watoto waanzishiwe vyakula vya nyongeza mara tu wanapotimiza umri wa miezi sita, kuanzia umri wa miezi sita wapewe vyakula vya nyongeza vyenye mchanganyiko wa makundi yote ya vyakula (kundi la nafaka, mizizi na ndizi za kupika,  kundi la vyakula vya asili ya wanyama, samaki na mikundekunde, kundi la mbogamboga, kundi la matunda, kundi la mafuta, sukari sambamba na kuendelee kunyonyeshwa maziwa ya mama hadi wafikie umri wa miaka miwili au zaidi kwa kadiri ya mama au wazazi watakavyoona inafaa.

Kuhusu faida za unyonyeshaji maziwa ya mama Dkt Magige anasema unyonyeshaji watoto maziwa ya mama ukifanyika ipasavyo familia, jamii na taifa kwa ujumla watapata faida ikiwemo watoto wachanga kuwa na hali nzuri ya lishe itakayo boresha ukuaji na maendeleo yao kimwili na kiakili, kasi ya watoto kupata magonjwa hatari ya kuambukizwa itapungua na hivyo kupunguza vifo vya watoto nchini, hali ya lishe na afya ya wanawake itaboreka kwa kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti na via vya uzazi; pamoja na kuepuka kupata mimba nyingine katika kipindi cha miezi michache baada ya kujifungua.

Mbali na hilo gharama za matibabu zitapungua kutokana na kuimarika kwa kingamwili kwa watoto hali itakayosababisha kupungua kwa kasi ya watoto kuugua mara kwa mara, tija katika shughuli za uzalishaji mali itaongezeka kutokana na wazazi kutumia muda mwingi katika kufanya kazi za kuongeza pato la familia badala ya kutumia muda huo kuuguza watoto na wanawake wanaonyonyesha watazidi kujiamini kuwa wanaweza kuwanyonyesha watoto wao vizuri kutokana na kutambua kuwa jamii ipo tayari kuwasaidia ili waweze kufanikisha unyonyeshaji inavyopaswa.

Afisa lishe Dkt Magige anasema athari/changamoto zitokanazo na kutokunyonyesha maziwa ya mama kikamilifu zipo za muda mrefu na mfupi zikiwemo watoto  kudumaa kimwili na kiakili na hivyo kupunguza kiwango chao cha kujifunza na kutambua mambo mbalimbali, na hatimaye kuwapunguzia fursa ya kupata elimu bora, na fursa ya kupata kipato kikubwa katika siku za usoni, viwango duni vya unyonyeshaji huchangia kuongeza kasi ya magonjwa miongoni mwa watoto wachanga na wadogo na  hivyo kuongeza gharama za matibabu na huduma za afya pia hupunguza muda wa wazazi au walezi kufanya kazi nyingine za kujipatia kipato na kujikimu kimaisha.

Amina Maduhu ni mama anayenyonyesha anasema watoto wake wawili amewanyonyesha bila kuzingatia taratibu za unyonyeshaji kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha hali iliyopelekea mmoja kati ya watoto wake kupata utapiamlo lakini kwasasa amepata elimu ambayo itamwezesha mwanaye wa mwezi mmoja kunyonya kikamilifu ikiwa ni sambamba na kumuanzishia chakula cha nyongeza pindi atakapofikisha umri sahihi wa uhitaji huo.

Bahati Kwilasa anasema ameanza kupata elimu ya namna ya kumyonyesha mtoto wake kliniki lakini pia alipata elimu mara baada ya mtoto wa jirani yake kulazwa kutokana na kuwa na utapiamlo ambapo amesema mama huyo alivyotoka hospitalini aliwaambia changamoto za kutokunyonyesha, kumuanzishia motto vyakula kabla ya umri wake sambamba na kutompatia mtoto vyakula vya nyongeza pindi tu anapofikisha umri wa miezi sita.  

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma