skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew amewataka wananchi wa mkoa wa Kigoma kutunza miundiombinu ya Anwani za Makazi kwa manufaa ya mkoa na nchi kwa ujumla.

Akizungumza leo mkoani humo, wakati akikagua utekelezaji na uhamasishaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi, Naibu Waziri huyo aliwataka wananchi hao kuhakikisha wanatunza miundombinu iliyowekwa ambayo ni vibao na nguzo vyenye majina ya mitaa, namba zilizoandikwa au kubandikwa katika majengo yao kwa lengo la kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa urahisi zaidi.

“Hizi namba ni kwa ajili ya manufaa ya wananchi, zimewekwa ili kurahisisha utoaji huduma mfano ikitokea mwananchi unahitaji huduma polisi basi unaweza kuwatajia namba na wakafika nyumbani kwako na kutoa msaada unaohitaji, lakini pia itasaidia kufikishiwa huduma zigine za maji, umeme na mawasiliano” Alisema Naibu Waziri Kundo

Alisisitiza “Tuchukulie miundombinu hii kwa umakini, nchi zilizoendelea mfano China, Marekani, Uswisi wao wamepiga hatua na hivyo na sisi lazima tujitahidi kufika huko lakini tutunze miundombinu hii na tuokoe fedha kwa ajili ya maendeleo yetu”.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mjini, Ester Mahawe alisema kuwa mkoa wake umetoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu faida na utunzaji wa miundombinu ya Anwani za Makazi na watachukua hatua kwa wananchi watakaoharibu miundombinu hiyo.

“Naomba hawa wanaoharibu miundombinu hii niwachukulie hatua kwa kuwa haya ni maelekezo ya Mhe. Rais na sisi tutatekeleza kwa kuhakikisha miundombinu hii inalindwa na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.” Alisisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma