Na. Ashura Ramadhani Waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu Kazi,Vijana, Ajira na watu wenye…
Wananchi mkoani Katavi wameilalamikia serikali kutokana na miundombinu chakavu na huduma mbovu zinazotolewa kwenye kituo cha usafiri wa gari moshi wilayani Mpanda ikiwemo kukosekana kwa jengo la abiria tangu huduma ya usafiri wa gari moshi ianzishwe miaka 50 iliyopita.
Wamesema kuwa kukosekana kwa jengo la abiria kunasababisha abiria kukosa hifadhi kipindi cha kusubiri usafiri jambo ambalo linaleta adha na usumbufu hasa kwa akina wenye watoto wadogo.
Akizungumza kwa niaba ya wasafiri Anna John amesema kuwa changamoto zaidi huwa kipindi cha masika na kuiomba serikali iwasaidie kuboresha huduma za reli ikiwemo jengo la abiria.
“Nililala nje nikisubiri gari moshi nikiwa na watoto wawili, mvua ikanyesha usiku kucha, sikuwa na jinsi ya kufanya, nilipata changamoto na watoto kiasi cha kupata homa, tunaomba serikali itusiadie tupate jengo la wasafiri kwaajili ya kujihifadhi” Ameeleza John
Naye William Benedicto amesema kuwa, kukosekana kwa jengo hilo kunapelekea abiria kusimama kwa muda mrefu wanapokua kwenye foleni ya kukatiwa tiketi, na mara nyingine kulowana kwa mvua kipindi cha msimu wa masika.

Kwa upande wake mkuu wa kituo cha reli Emmanuel Mtawali amezungumzia uhaba wa mabehewa kutoka Mpanda kwenda Dar-es- unasababisha abiria kubanana ndani ya behewa moja jambo ambalo linaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa.
“Hadi sasa tuna mabehewa matatu yatokayo Mpanda kwenda Dar-es-Salaam, hayatoshi, yanaleta msongamano mkubwa wa abiria, inabidi yaongezeke mabehewa mengine mawili ili kukidhi haja ya wasafiri” Alisema Mtawali
Akilizungumzia hilo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mwita Waitara alipotembelea kituo hicho alimtaka mtendaji mkuu kutoa majibu lini jengo la abiria litajengwa.
“Jambo hili halikubaliki na imenipa picha kuwa hizi stesheni zote inabidi zikaguliwe inawezekana hali ni mbaya maeneo yote, hata hali ya usafi wa jengo ni mbaya, linanuka na halifai kwa matumizi ya binadamu, kwani bajeti ya kusafisha hapo nikiasi gani?, alihoji Waitara.
Mwandishi: Neema Hussein
Mhariri: Adela Madyane