skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Wahariri kutoka vituo mbalimbali vya Radio nchini Tanzania wamehimizwa kutumia nafasi waliyonayo ya kuaminiwa na wananchi kufikisha taarifa sahihi za sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti mwaka huu

Rai hiyo imetolewa katika mafunzo yanayoendelea mkoani Iringa na Mtalaam wa idadi ya watu kutoka ofisi ya taifa ya takwimu Bi. Helen Hilary wakati akitoa mada ya umhimu wa sensa na namna itakavyofanyika sambamba na wajibu wa vyombo vya habari vya kijamii.

Imeelezwa kuwa, matokeo ya sensa ni dira sahihi ya mipango ya maendeleo na yatatumika kubuni na kuandaa sera mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya jamii ikiwemo Afya, elimu, miundombinu na uchumi utakaokuwa jumuishi na wenye kugusa mahitaji ya watu katika maeneo husika.

Helen Hilary Mtalaam wa Idadi ya watu kutoka Ofisi ya taifa ya takwimu

Bi. Hilary amesisitiza kuwa vyombo vya habari hasa vya kijamii vinaaminiwa na wananchi na vinasikilizwa sana ukilinganisha na vyombo vingine vya kitaifa, hivyo hiyo iwe fursa kwa redio jamii katika usambazaji wa habari kuhusu sensa ya watu na makazi.

“Tunatambua kuwa redio zenu zinasikilizwa sana na kuaminika, hivyo imani ya jamii kwenu itumike pia kuwapa elimu juu ya sensa na kuwahamasisha kujitokeza kushiriki katika zoezi hili mhimu kwa maendeleo ya taifa letu”. amesisitiza Helen Hilary

Wahariri wakisikiliza kwa umakini mawasilisho kutoka kwa wataalam kutoka Ofisi ya mtakwimu mkuu wa serikali kuhusuu Sensa ya watu na makazi 2022

kwa upande wake Mwalimu wa uandishi wa habari kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam Mwalimu Darius Mukiza amewahimiza waandishi wa habari kuwa na fikra dadisi kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii ili kupata takwimu sahihi zitakazotumika kuleta mageuzi katika jamii husika

“Waandishi wengi hawana tabia ya kudadisi masuala ya takwimu, mfano serikali ilitangaza ongezeko la mishahara, hakuna chombo kilichodadisi ni kiasi gani kitapanda, pia serikali ilitangaza kutoa pesa kuwezesha bei ya mafuta kuwa himilivu lakini hakuna chombo kilichoandika uchambuzi wa kitakwimu kuhusu tija hiyo” amesisitiza Mukiza

Bw. Mukiza amesisitiza kuwa pamoja na kuwepo na habari nyingi za kitakwimu vyombo vingi na waandishi wake wa habari hawatoi kipaumbele cha kuandaa maudhui mahususi ya kitakwimu ikiwemo sensa.

Fikiria; serikali imetangaza kuwa elimu ya kidato cha tano na cha sita itakuwa bure, lakini huoni chombo kinachoandika uchambuzi kuhusu tija ya msamaha huo wa ada na kiasi gani kitatumika kulipia adaza wanafunzi wa madarasa hayo” amesisitiza Mukiza

Takribani wahariri 200 wa habari kutoka Radio mbalimbali za kijamii, kikanda na kitaifa wamehudhuria mafunzo maalumu kuhusu Sensa ya watu na makazi mwaka 2022.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma