Asema hadi sasa imeshawekeza dola za Marekani bilioni 10 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi…
SIKU YA WAKIMBIZI DUNIANI 2022- NYARUGUSU KIGOMA
Wakati dunia ikiadhimisha siku ya mkimbizi duniani, wakimbizi wa Burundi na DRC wanaoishi uhamishoni nchini Tanzania wameelezea kuridhishwa kwao na mwendendo wa amani katika nchi zao sambamba na huduma wanazopata ndani ya kambi kutoka kwa mashirika wahisani wa Umoja wa mataifa
Wakiongea mapema leo katika kambi ya Nyarugusu inayohifadhi wakimbizi kutoka Burundi na DRC magharibi mwa Tanzania wakimbizi hao wamebainisha kuwa, pamoja na kukosa uhuru kutokana na masharti ya nchi walimohifadhiwa, wanaridhishwa na huduma pamoja na usalama
Asokolo Atanga ambaye ni mkimbizi kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya congo anaiona siku ya mkimbizi duniani kama fursa kwao kutafakari kuhusu ukimbizi pamoja na misukosuko waliyokumbana nayo sambamba kujenga fikra za pamoja kurejea nchini mwao
Wakimbizi kwa pamoja wametaja kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamekuwa ya tofauti ukilinganisha na mwaka 2020/2021 ambapo walisherehekea wakiwa katika mbinyo wa kunyimwa haki mbalimbali ikiwemo ya kuzuiliwa kutumia vyombo vya usafiri kambini, pamoja na kuwepo kwa matukio ya uhalifu hususani ukatili kwa Watoto na wanawake.
Baruani mayaya ni shuhuda wa mabadiliko hayo na anataja kuwa vitendo vya uhalifu hususani ubakaji wa wasichana umedhibitiwa na kwamba huduma za usafiri wa baiskeli zimerejeshwa jambo linalosaidia wao kupata huduma za kijamii
Kinachofurahisha wengi ni mtazamo mpya wa wakimbizi kutoka Burundi ambao wengi wanakiri kuwa kwa sasa nchi yao ina amani ukilinganisha na miaka miwili iliyopita hali inayohamasisha wengi wao kuhiyari kurejea. Hata hivyo mama huyu aliyejitambulisha kwa jina la Kigeme Joseline anakili kutokuwa tayari kurejea kwa kile anachodai kuwa na migongano mingi katika jamii katika maeneo waliyoyahama kukimbia machafuko mwaka 2020.
Joseline anatumia siku ya wakimbizi kuomba serikali ya Tanzania kumwacha asalie kambini hapo au kumtafutia makazi mengine badala ya kumhamasiaha kurejea Burundi

Katibu tawala wa wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma Bw. Titus Mguha ambaye ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya leo, amewahimiza wakimbizi kutunza amani na kuendelea kufikiri kurejea katika nchi zao kama suluhisho la kudumu la ukimbizi wao
Kwa upande wake mkuu wa UNHCR wilayani Kasulu Bw. Ben Dialo amewataka wakimbizi kuwa wavumilivu kwa kuishi katika utulivu kwakuwa dunia kwa sasa kuna kundi kubwa la wakimbizi duniani ambapo taaarifa za mwaka huu zinaripoti uwepo wa wakimbizi wapatao milioni 100, na kundi jipya ya wakimbizi milioni 13 kutoa Ulaya ambao wote wanahitaji misaada ya kiutu kama ilivyo kwa wakimbizi waliopo Tanzania.
Dialo ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kuimarisha ulinzi wa wakimbizi wote na kuhakikisha huduma za kiutu zinapatikana.
Imeandaliwa na Adela Madyane, Nyarugusu
Imehaririwa na Prosper Kwigize