skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki, Bariadi

Jumla ya vikundi 13 vya wanawake ,vijana na watu wenye ulemavu vilivyopo halmashauri ya wilaya ya Bariadi vimepokea vifaa mbalimbali ikiwemo vyerehani,mizinga ya kufugia nyuki, pikipiki kwaajili ya bodaboda na mashine ya kukamulia mafuta vyote kwa ajili ya kukuza kipato.

Vifaa vilivyotolewa vina thamani ya kiasi cha shilingi milioni 130 pesa ambazo kimetokana na makusanyo ya mapato ya ndani ya halmashauri ya wilaya ya Bariadi na ni kwa ajili ya vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wilayani hapo.

Akikabidhi vitendea kazi hivyo vya ujasiriamali, mkuu wa wilaya ya Bariadi ndugu Simon Simalenga ya Bariadi amesema mapato yakikusanywa kwa wingi yatatoa wigo mpana kwa idadi ya vikundi vitakavyokopeshwa kupitia asilimia kumi ya mapato hayo kuongezeka.

“Tukusanye mapato haya yawe mengi,fedha hizi zikiwa nyingi kwa upande wa halmashauri maana yake tutatoa wigo mpana kwa vikundi mbalimbali kupata mikopo kwasababu asilimia itakuwa imeongezeka” amesema Simalenga.

Mkuu wa wilaya ya Bariadi Comrade Simon Simalenga akipanda moja ya pikipiki zilizotolewa kwa kikundi cha vijana

Aidha amevipongeza vikundi vilivyopata mikopo huku akiongeza kuwa vipo vikundi vingi kwenye halmashauri hiyo ambavyo vipo hai na vingi vina sifa ya kupata mikopo hivyo kupitia ukusanyaji wa mapato kikamilifu kutaviwezesha kupata kwa vingi zaidi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri hiyo Lucas Mayala amesema wana jumla ya kata 21 na kwenye kata moja vinaweza kuwepo vikundi zaidi ya 30 na vyote vimesajiliwa.

” Ukipiga hesabu ya kata 21 na vikundi vyake utakutana na vikundi zaidi ya 600,na hivyo kuona mahitaji ni makubwa sana kuliko kile kipato tunachokipata cha asilimia 10″amesema Mayala.

Aidha Mayala ameongeza kuwa vikundi hivyo vinavyopata mkopo vimetoka kwenye kata sita kati ya 21 na hivyo kwenye robo ya kwanza vitafikiwa hivyo vichache na robo nyingine zitakopeshwa kata zingine.

Kikundi cha Vijana wanaojishughulisha na ufugaji wa nyuki, wakikabidhiwa Mizinga ya kisasa na mavazi maalumu ya ulinaji wa asali

Awali akitoa taarifa kwenye hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii Beatrice Gwamagobe amesema kwa mwaka wa fedha 2022/23 halmashauri hiyo ilipanga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 1.9 na kitenga kiasi cha milioni mia moja tisini na moja ambayo ni asilimia 100 ya mapato hayo kwaajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya ujasiliamali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu .

Gwamagobe amesema hadi kufikia Disemba 31,2022 halmashauri hiyo ilikusanya kiasi cha shilingi bilioni moja sawa na asilimia 53 ikiwa ni mapato yasiyolindwa na kupeleka kwenye akaunti maalum ya vikundi kiasi cha shilingi milioni 60 kwaajili ya kuvikopesha vikundi.

Pamoja na hayo amesema kiasi cha shilingi milioni 59 kimekopeshwa kwa vikundi viwili vya wanawake, kimoja cha vijana na mtu mwenye ulemavu mmoja huku kiasi cha shilingi milioni moja kikibaki kwenye akaunti kwaajili ya kukopesha vikundi mara baada ya taratibu kukamilika kwenye robo ya tatu.

Nao baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo akiwemo Kanengo Gada na Nsulwa Malugu wameahidi kurejesha mikopo hiyo kwa wakati uliopangwa huku wakiongeza kuwa ni vema vikundi vyote vikajenga hali ya kuaminika kwani kurejesha kwa uaminifu na kuzingatia muda mbali na kupata zaidi pia kunawezesha vikundi vingine kupata fursa hiyo.

Jumla ya vikundi 13 vimepata mkopo wa vifaa vikiwemo 10 vya wanawake,vijana viwili na watu wenye ulemavu kimoja.
Aliyeshika mic ni mkuu wa wilaya ya Bariadi Simon Simalenga

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma