skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Matinde Nestory, Mwanza

Wakati kombe la dunia la wanawake likiendelea na mtifuano wake huko Morocco kwa wasichana kuonesha vipaji vya hali ya juu katika Soka, nchini Tanzania wito umetolewa juu ya kuyatumia mashindano ya michezo kwa shule za msingi kama kitovu na chimbuko la vipaji kwa wasichana katika fani mbalimbali za michezo.

Afisa Elimu msingi jiji la Mwanza Mwalimu Mussa Labwe amehimiza mwamko huo wakati akifungua mashindano ya UMITASHUMTA mkoa wa Mwaza ambayo yanafanyika siku mbili katika uwanja wa Nyamagana uliopo jijini Mwanza.

Amesema, washiriki wa mashindano ya wanafunzi wa shule za msingi yatumike kuhakikisha kunakuwepo na ushiriki thabiti wa watoto katika fani hiyo, akisisitiza kuwa michezo ni ajira ,afya pamoja na kuleta watu pamoja kwa kuonesha vipaji na kuhakikisha vinalelewa na kufika mbali. 

Mwalimu Mussa Labwe (mwenye tracksuit ya njano) akisalimiana na moja ya timu inayoshiriki mashindano ya shule za msingi Jijini Mwanza

Mwalimu Labwe amesema kuwa  kipaji ni ajira inayodumu na kuwaleta watu pamoja katika kuburudika na  lengo la mashindano ni kuandaa timu moja ya kuwakilisha wilaya ya Nyamagana ambayo itashindana na halmashauri zingine na kutengeneza timu ya Mkoa.

“Niwaombe kwa yeyote ambaye amekuja kushindana hapa ajiibidishe tunahitaji Kupata vipaji kweli kweli kwa ajili ya kutuwakilisha jiji la mwanza na wale wanaojua kucheza ndio watachukuliwa tumejipanga kuchagua timu bora na yenye ushindani” amesema Afisa Elimu Labwe.

Kwa upande wake Afisa utamaduni jiji Agnes Majinge amesema mashindano hayo ni kwa ajili ya kutengeneza timu ambayo vipaji vitavumbuliwa  na kuendelezwa  katika fani mbalimbali za Sanaa.

“Mtoto mwenye kipaji tutahakikisha kipaji kile tunakilea na kukiweka kuonekana mpaka kwenye ngazi ya taifa na hata ngazi ya kimataifa pamoja na tunahakikisha wale watakaoonyesha vipaji vyao watachaguliwa na kwenda kuwakilisha Mkoa”amesema Majinge.

Afisa Utamaduni Mkoa wa Mwanza Mwl. Agnes Majinge (wa kwanza kushoto) na Afisa Michezo Bw. Mohamed Bitegeko (wapili kulia) wakiungana na walimu mbalimbali pamoja na moja ya timu za watoto katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa mashindano.

Nae Afisa michezo jiji Mohamed Bitegeko amesema kuwa kata 18 za halmashauri ya jiji wameshiriki katika mashindano hayo  na kuzipanga  timu katika Kanda nne  nne ambazo ni kwa ajili ya  kuunda timu ya halmashauri ya jiji la Mwanza ambazo ni  timu ya Mpira wa soka, Netball, Volleyball,Handball,Goliball,Riadha ambapo Kuna mbio,miruko na mitupo,fani za ndani ambapo Kuna ngoma,kwaya na muziki pamoja na soka maalumu kwa ajili ya viziwi.

“Kwenye uchaguzi wa uteuzi wa wachezaji watakaoshiriki katika kutengeneza timu ya Mkoa tutashirikiana kwa karibu Sana na vyama vya michezo na Walimu wenyewe wanashiriki kwa kiwango kikubwa Kupata timu bora ili kuepuka malalamiko”amesema Bitegeko.

Baadhi ya washiriki kutoka shule ya msingi Buhongwa na Shamaliwa wamesema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi ili wapate nafasi ya kuchaguliwa katika timu ya wilaya pamoja na kupeperusha bendera ya  jiji la mwanza katika kuchukua kombe pamoja na kujitangaza kimataifa.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma