skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mwandishi wetu

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga ameeleza kuwa, Serikali
kupitia Wakala wa Nishati Vijijini inatekeleza Mradi wa Kusambaza
Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ambapo vijiji vyote
ambavyo havina umeme Tanzania bara vitafikiwa na huduma ya umeme.

 Ameeleza hayo bungeni, jijini Dodoma tarehe 6 Septemba, 2023 wakati
akijibu swali la Mbunge wa Masasi, Mhe.Geofrey Mwambe ambaye alitaka
kujua ni  lini Serikali itapeleka umeme kwenye Vijiji vya Namikunda,
Chipole, Machombe, Mtakateni, Machenje, Matawale, Mpekeso, Chakama na
Kata ya Temeke.

 Akijibu swali hilo, Mhe.Kapinga amesema kuwa  katika Jimbo la Masasi,
Mkandarasi NAMIS Corporate Limited alipewa jumla ya vijiji 17 ambavyo
havikuwa na umeme ambapo hadi kufikia tarehe 15 Agosti 2023, vijiji 11
vimeshawashwa umeme na vijiji 6 vitakamilika kabla ya mkataba wa
Mkandarasi kuisha tarehe 31 Desemba, 2023.

 Ameongeza kuwa, vijiji vya Namikunda, Mtakateni, Matawale, Mpekeso na
Chakama vimekwishawashwa umeme. Vilevile, hadi kufikia tarehe 31
Desemba 2023, Vijiji vya Chipole na Machombe vitakuwa vimepatiwa
umeme.

Amesema kuwa, kwa sasa, zoezi la kusimamisha nguzo katika Kata ya
Temeke (Mkarango) bado linaendelea na  nguzo tayari zimekwisha
simamishwa katika kijiji cha Machenje na zoezi la kuvuta waya
linatarajiwa kufanyika mwezi Septemba, 2023.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma