skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki ,Bariadi

Katika kuhakikisha wanafunzi wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2023  wanapata nafasi kwenye  shule za kutwa  tayari mkoa wa Simiyu umepokea kiasi cha shilingi  bilioni 4.78. kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 239.

Ujenzi wa vyumba hivyo ulianza Oktoba 2022 na unatarajia kukamilika Desemba 15, 2022 na hadi kufikia Novemba 22,2022 jumla ya vyumba vinne vya madarasa vimekamilika, vyumba 104 vipo katika hatua ya  ukamilishaji, vyumba 50 hatua ya upauaji, vyumba 61 hatua ya lenta, vyumba 16 hatua ya boma na vyumba vinne hatua ya hatua ya msingi .

Hayo yamesemwa na katibu tawala wa mkoa wa Simiyu Prisca Kayombo wakati akitoa taarifa ya mkoa huo ambayo ameiwasilisha kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo Dkt Yahaya Nawanda mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) Angellah Kairuki ambaye yupo kwenye ziara ya kikazi mkoani hapo.

katibu tawala wa mkoa wa Simiyu Prisca Kayombo wakati akitoa taarifa ya mkoa huo

Kayombo amesema vyumba hivyo vikikamilika vitawezesha wanafunzi wote watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2023 kupata nafasi katika shule za sekondari za kutwa huku akigusia changamoto wakati wa ujenzi ambazo ni pamoja  upandishaji wa bei za vifaa vya ujenzi, uhaba wa mafundi wa ujenzi kwa baadhi ya maeneo mkoani hapo, uhaba wa maji hususan katika halmashauri ya Meatu.

Mara baada ya kupokea taarifa waziri Kairuki ametaka kazi za ujenzi wa vyumba hivyo uendelee kufanyika kwa kasi ya juu ikiwa ni sambamba na kuzingatia ubora wa hali ya juu ili majengo hayo yadumu kwa ajili ya manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

” Tunakuja na majengo mengi kuanzia Januari…serikali ya mama Samia  inaendelea kutoa fedha…. cha msingi ubora na kasi ya juu ya hali ya juu mzingatie katika ujenzi wa majengo haya  Tanzania ni nchi kubwa tunataka jengo litakalokaa miaka 50..75 mpaka 100″amesema waziri Kairuki .

Katika hatua nyingi waziri Kairuki amesema serikali itaendelea kutoa pesa za ujenzi wa shule moja kwenye kila  halmashauri nchi kupitia mradi wa kuimarisha na kuboresha elimu ya sekondari ambapo kila halmashauri itapata kiasi cha shilingi milioni 600.

” Tumekuwa tukileta shule mbalimbali kupitia mradi wa kuimarisha na kuboresha elimu ya sekondari kwa halmashauri yenu pia mwaka huu tulionao unaomalizika  Juni tutaleta shule nyingine moja… kwa halmashauri milioni 600 na tutafanya hivyo mpaka 2025 kwa takribani miaka  minne tutaendelea kuhakikisha kila mwaka tunafanya hivyo na hii ni kwa nchi nzima …  tutakapoletewa fedha hizo tutimize wajibu wetu tutumie fedha hizo vizuri..thamani halisi ya fedha ionekane, ubora lakini pia na kasi ya ujenzi ionekane pasipo kuathiri ubora wa majengo yetu” amesema waziri Kairuki.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma