Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi kama ifuatavyo:…
Na. Matinde Nestory, Mwanza
Shirikisho la vyama vya wafanyakazi (TUCTA) Mkoa wa Mwanza limempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ongezeko la mshahara wa asilimia 23.3 kwa watumishi wa umma wakidai kuwa serikali imesikiliza kilio chao cha muda mrefu.
Pongezi hizo zimetolewa jijini Mwanza likienda sambamba na maandamano ambayo yameongozwa na Mkuu wa wilaya ya Nyamaga Amina Makilagi kuanzia katika uwanja wa Grand hall na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Engineer Robert Gabriel katika ofisi za Mkuu wa Mkoa.
Akisoma risala kwa niaba ya wanachama, katibu wa TUCTA Mkoa wa Mwanza Bw. Zebedayo Athuman amempongeza Rais Samia kwa kuongeza mishahara kwa wafanyakazi wa umma kakidai kuwa ongezeko hilo litawakwamua kiuchumi.

Aidha TUCTA imepongeza Serikali kwa kuwapandisha vyeo watumishi wa umma 92619 na kuajiri watumishi wapya 12336 jambo ambalo linatajwa kupunguza uhaba wa watumishi nchini hasa katika sekta ya Elimu na Afya
Wakati huo huo, watumishi wa umma walioshiriki maandamano hayo ya pongezi wameziomba taasisi binafsi kufikiria namna ya kuboresha maslahi ya watumishi wao ili kuongeza ufanisi katika kazi zao. huku Mwenyekiti wa TUCTA mkoa wa Mwanza Bw. Yusuf Simbaulanga akiihakikishia serikali kuwa shirikisho hilo litakuwa bega kwa benga na serikali katika kuwatumikia wananchi
“Sisi TUCTA Mkoa wa Mwanza tunaomba jitihada zilizofanyika katika sekta ya umma zifanyike haraka kwa wafanyakazi wa sekta binafsi ambao nao wanastahili kuongezewa mishahara” amesema katibu TUCTA Atuman.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Mwanza Engineer Robert Gabriel ambaye alikuwa mgeni rasmi, amewataka wafanyakazi wote mkoani Mwanza kufanya kazi kwa uadilifu na kuhakikisha wanatimiza malengo kwa serikali na kwa wananchi na kuhakikisha hawajihusishi na ubadhirifu wa Mali pamoja na kuepuka vitendo vya rushwa.

Mmoja wa walimu kutoka jiji la Mwanza Vivian Nyambui amepongeza na kumshukuru Rais Samia kuwarudisha shuleni wanafunzi waliopata ujauzito.