Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi kama ifuatavyo:…
Adela Madyane- Kigoma
Wito umetolewa kwa wananchi kutokwenda kwenye vituo vya afya ambavyo havisajiliwa na serikali na ambavyo havina wataalamu vyenye mlengo wa kibiashara ili kuepuka kupewa mlundikano wa dawa usioendana na ugonjwa husika.
Umetolewa na MENEJA wa kanda ya magharibi wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Christopher mi Migoha wakati wa ziara ya wajumbe wa bodi ya TMDA mkoani Kigoma kwa lengo la kuangalia utendaji kazi, changamoto zilizopo na kutambua takwimu za uingizaji wa bidhaa ambazo haufuati taratibu za kisheria ambapo walitembelea katika maeneo ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni , bandarini pamoja na mpakani mwa Burundi na Tanzania.
“Wananchi wasiende sehemu ambayo wataalamu wake wanafikiria biashara zaidi kuliko kutoa huduma na ikitokea mtu amelundikiwa dawa au kupewa huduma mbaya atoe taarifa kwenye bodi ya TMDA au kwa mganga mkuu wa mkoa au wa wilaya kwaajili ya mtaalamu huyo kupelekwa kwenye bodi ya taaluma ili achukuliwe hatua za kisheria” Ameelekeza Migoha.

Migoha amesistiza zaidi kuwa ni muhimu wataalamu wakafanya kazi kulingana na maadili ya kitaaluma yanavyoelekeza ili wagonjwa wapewe dawa sahihi kwa ugonjwa sahihi na kwa kupima kipimo sahihi.
Akizitaja baadhi ya changamoto wanazopata wakati wa ukaguzi Meneja kanda amesema ni kwa baadhi ya wauzaji wa maduka ya dawa muhimu kuuza dawa ambazo haziruhusiwi na zilizokwisha muda wake huku wengine wakiuza madawa ya serikali kinyume na taratibu za utunzaji wa dawa.
“Ni wachache wanaouza dawa zilizopitwa na muda wake, ila kwa kitendo chochote cha ukiukwaji wa maadili tunachukua hatua za kisheria za kuziondoa dawa sokoni na kwenda kuziharibu na muhusika atalazimika kulipia gharama za uharibuji wa dawa hizo kwa mujibu wa sheria”Amesema Meneja kanda.

Naye mkurugenzi mkuu wa TMDA Adam Fimbo ameridhishwa na hali halisi kwamba hakuna takwimu zinayoonesha uingizaji wa bidhaa bandia au duni kupitia mpaka wa Manyovu uliopo wilayani Buhigwe na kuamini kwamba wananchi wanapata bidhaa bora jambo ambalo limetimiza lengo la mamlaka hiyo la kuhakikisha mtumiaji wa mwisho anapata bidhaa bora sambamba na kudhibiti uingiaji ambao haufuti utaratibu wa sheria na kanuni katika mipaka yote 32.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa bodi hiyo Erick Shitindi ameshauri kuwa eneo la kuchoma takataka zisizotakiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni liboreshwe kwa teknolojia nzuri zaidi ili kupungaza moshi unaoweza kuwaathiri binadamu wanaopita katika eneo hilo na wanaoishi maeneo ya jirani.