skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Adela Madyane-Kigoma

Mkuu wa shule ya sekondari ya Lagosa Sofia Theobald, iliyopo kata ya Igalula wilayani Uvinza mkoani Kigoma amekiri uwepo wa bweni umeweza kumaliza changamoto za mimba, utoro na kuongeza ufaulu wa watoto wa kike waliopo shuleni hapo.

Ameyasema hayo katika taarifa fupi aliyoiandaa kwa wageni wa shirika la The Nature Conservancy (TNC) walio wadhamini wa ujenzi wa mabweni ya wasichana katika shule hiyo

Amesema kwa kipindi cha mwaka 2016-2018 hakukuwa na mtoto wa kike aliyefaulu vizuri na idadi ya waliohitimu haikuzidi wanafunzi saba, ila baada ya upatikanaji wa bweni ufaulu umeongezeka mpaka kufikia kwa baadhi yao kupata daraja la pili na hakuna aliyepata zero.

“Tunaishukuru serikali na shirika la TNC kwakuwa ufaulu tunaoupata leo umetokana na juhudi zenu za kutuwezesha kupata bweni, upatikanaji wa umeme, maji safi na salama, pamoja na vifaa vya hedhi salama, mazingira ya kielimu yameboreka zaidi kwa jitihada zenu”Amesema Theobald

Mkurugenzi wa wa Tanzania wa shirika la The Nature Conservancy Lucy Magembe akizungumza na wazazi wakati wa matembezi shuleni Lagosa.

Naye afisa elimu sekondari kutoka wolaya ya Uvinza Magreth Kilenza amesema sekondari ya Lagosa imefanikiwa kuweka historia kwa watoto wa kike nane kupata daraja la pili kwa matokea ya 2020-2021 jambo ambalo halikuwahi kutokea katika wilaya ya hiyo.

“Kutokana na idadi kubwa ya watoto wa kike wanaoshindwa kuendelea na masomo tunajenga bweni la pili lakini pia kutokana na miundo mbinu ya shule iliyopo hapa serikali inapanga kuifanya Lagosa kuwa “A level”, na tutaweka uzio ili kuongeza usalama kwa watoto wetu” Amesema Kilenza

Akizungumza kwa niaba ya wazazi Konslida Kiza amewaomba wakurugenzi wa TNC kujenga bweni kwaajili ya watoto wa kiume kwani nao wanakutana na adha mbalimbali ikiwemo kutembea umbali mrefu takribani kilometa 50, mazingira hafifu ya kujisomea na ukosefu wa maji maji safi na salama.

Kwa upande wa Kezia Bandekuye mwanafunzi wa kidato cha nne shuleni hapo amesema amefanikiwa kuongeza ufaulu wake mara alipoanza kuishi bweni kutoka kuwa mwanafunzi wa 100 kati ya wanafunzi 120 hadi kuwa mwanafunzi wa 15 kati ya wanafunzi 88 na kuamini kuwa matokeao hayo yatamuwezesha kuendelea na elimu ya juu.

Mandhari ya shule ya sekondari Lagosa

Naye Yohana Agustino mwanafunzi wa kidato cha nne kutoka kijiji cha Igalula amesema imewabidi kuweka makambi maeneo ya karibu na shule kwaajili ya kupata nishati ya umeme ili kujiandaa kwaajili ya mitihani inayowakabili na kuiomba serikali kuwajengea bweni ili kupunguza changamoto hizo ambazo huongezeka zaidi kipindi cha masika

Kwa upande wa mkurgenzi wa shirika la TNC nchini Lucy Magembe amesema kuwa iliwapasa kuanza na ujenzi wa bweni la wasichana kutokana na changamoto zao kuwa nyingi zaidi na kwamba wataongeza ushirikiano zaidi na jamii pamoja na serikali kwa maeneo ambayo yatahitaji ushirikiano huo.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma