skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Adela Madyane

Neema ya usafirishaji wa bidhaa mbalimbali imepatikana kwa wananchi zaidi ya 500 waliomo katika vikundi vya  uhifadhi vya kuweka na kukopa (COCOBA) na vikundi vya usimamizi wa rasilimali za ziwa  (BMU) baada ya kukabidhiwa bajaji za mizigo (guta) kumi zenye thamani ya shilingi milioni 75 katika kata ya Buhingu wilayani Uvinza mkoani Kigoma.

Ufadhili huo wa kipekee wa nyezo za usafiri umetolewa na shirika la The Nature Conservancy (TNC) kupitia mradi wa pamoja wa TUUNGANE  kwa lengo la kupunguza adha ya usafirishaji wa mazao kutoka shambani kama vile mpunga, mahindi, mihogo na maharage  pamoja na mazao ya ziwa Tanganyika ya samaki na dagaa kutoka mwaloni kuelekea barabarani  kwaajili ya kusafirishwa kwenda katika masoko ya ndani na nje ya mkoa.

Wakizungumza baada ya kukabidhiwa bajaji hizo na mkuu wa Wilaya ya Uvinza Dinnah Mathamani, wananchi wa Buhigu wamesema bajaji hizo zitawawezesha kuongeza kipato cha kikundi na cha mtu mmoja mmoja na kuwa sambamba na kutumika katika shughuli za kikundi zitatumika pia kama kitega uchumi kwa kubeba mizigo ya watu wengine kutoka kijiji kimoja hadi kingine.

 Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Dinnah Mathamani akijaribu uzima wa bajaji kabla ya kuzikabidhi kwa wana kikundi eneo la sokoni kata ya Buhingu.

Kwa niaba ya wanakikundi wa Upendo COCOBA, Zainab Katumba amesema walitumia usafiri wa boda boda kusafirisha mizigo yao uliowagharimu kiasi cha shilingi 40,000 kwa gunia moja la dagaa kutoka mwaloni kuelekea vijiji vya jirani kwaajili ya masoko vyenye takribani umbali wa kilomemeta 40 na bei kupanda kulingana na umbali na kwamba uwepo wa bajaji utapunguza gharama hizo zitazosaidia kwenye matumizi  mengine.ya familia.

Kwa upande wake mwenyekiti wa BMU kata ya Buhingu Richard Nkayamba amesema, uwepo wa Bajaji utarahisisha kusafirisha mazao ya samaki na dagaa zilizochakatwa na kupakiwa kwa wingi katika maeneo ya barabarani ili kusafirishwa katika masoko makubwa na kwa haraka, hivyo kuongeza kipato katika jamii kwani kuna tofauti ya kipato kwa kuuza kwenye masoko ya ndani ya wilaya na masoko ya nje ya wilaya na mkoa kwa jumla.

Naye Mkuu wa wilaya ya Uvinza Dinna Mathamani amesema bajaji hizo ni mali ya kikundi, hivyo zitumike kwa malengo kusudiwa ya kikundi ili zitumike kuongeza kipato katika kaya sambamba na kutunza mazingira.

Mathamani alitoa maelekezo kwa  wanakikundi kutunza bajaji hizo  na ziendeshwe na madereva wenye sifa hususan wenye leseni na zitumike kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi na kuwataka viongozi wa vikundi kuisimamia kwa mujibu wa katiba yao ili kuepuka kuwa chanzo cha mgogoro katika vikundi.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma