skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Adela Madyane-Kigoma.

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kituo cha Kihinga mkoani Kigoma imesema baada ya miaka saba Tanzania itakuwa imejitosheleza kwa mafuta ya kula na kuacha kuagiza nje ya nchi jambo ambalo litaiondolea serikali gharama ya kuagiza tani 360 za mafuta zenye gharama ya shilingi bilioni 470 kila mwaka.

Hatua hiyo imekuja baada ya kituo hicho kuongeza uzalishaji wa mbegu za kisasa za michikichi aina ya tenera na wananchi kuitikia uzalisha wa kutumia mbegu hizo zenye uwezo wa kuzalisha tani 4.5 za mafuta kwa hekta moja tofauti na mbegu za zamani za jiwe ambazo hutoa tani 1.6.

Akizungumza na Nipashe Kuzenza Madili afisa kilimo na mratibu wa uzalishaji wa teknolojia na mahusiano kituo cha TARI Kihinga alisema mpaka sasa kituo hicho kimeshazalisha mbegu milioni 14,444,000 na kusambaza mbegu miloni 11,899,000 katika halmashauri za mkoa huo na taasisi nyingine za umma ikiwemo za kikosi cha 821 cha jeshi la kujenga Taifa (JKT),cha Bulombora ,magereza ya Ilagala, magereza ya Kwitanga, taasisi ya Undugu pamoja na wakala wa mbegu Tanzania (ASA) na mikoa mingine kote nchini.

“Kati ya mbegu hizo tulizozalisha tumeweza kupata miche 3,206,000 ambayo kati ya hiyo, miche 1,968,000 ilishapandwa huku mingine ikiendelea kuhudumiwa katika kitalu, upandaji wa miche hiyo umewezesha kupata eneo jipya lililopandwa miche ya kisasa ya tenera hekta 21,000 kwa msimu uliopita wa mwaka 2021-2022 katika halmashauri zote nane na taasisi za serikali zilizopewa dhamana ya kusimami zao la mchikichi.” Alisema Kuzenza

Sehemu ya kitalu cha uzalishaji wa miche ya michikichi katika shamba la JKT Bulombora mkoani Kigoma

Alisema hatua hiyo imepunguza changamoto kubwa ya upatikanaji wa miche za mbegu bora ambazo serikali imegharamia na wananchi kupewa mbegu bure kwaajili ya kuziendeleza na kuhakikisha tatizo la mafuta linakwisha kabisa nchini na kuanza kuuza nje ya nchi.

Alisema mbali na halmashauri nane za mkoa wa Kigoma, hamasa za kulima zao hilo zimesambaa mpaka kwa wakulima nje ya mkoa huo kote nchini ambapo halmashauri 26 za mikoa ya Pwani, Mbeya, Dar-es-Salam, Katavi, Mtwara wamehamasika kulima zao hilo jambo linalooshiria kuongezeka kwa uzaishaji wa mafuta

Kuzenza alisisitiza kuwa ili mafuta yaweze kutosheleza ndani ya miaka hiyo, mbinu ya kutoa elimu bora ya namna ya kutunza vitalu na utunzaji wa mchikichi, imetolewa kwa maafisa ugani 1825 kote nchini katika mikoa inayolima zao la mchikichi ili kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wakulima ili kuongeza uzalishaji.

Kwa uapande wa mkurugenzi wa TARI, kituo cha Kihinga Filson Kagimbo alisema endapo wananchi watahamasika na kulima hekta laki moja za mchikichi ambazo ni sawa na tani 600,000 za mafuta kwa mwaka kwa wastani wa tani 4.5 za mafuta kwa hekta, serikali itakuwa imeokoa ghrama hizo na kuwaomba wananchi kote nchini kwenye hamlsahauri ambako hali ya hewa inaruhusu kulima zao hilo kuanza kilimo bila kusita.

Kagimbo alisema zao la mchikichi Iimeanzishwa mahususi kwaajili ya kutatua tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula hapa nchini Tanzania, kwani kwa sasa nchi inatumia tani 650,000 kwa mwaka na uwezo wa kuzalisha kuwa tani 290,000 sawa na asilimia 44.6 na kuacha upungufu wa tani 360,000 zinazogharimu bilioni 470 na kutoa wito kwa jamii nzima na wawekezaji uchangamkia fursa ya kilimo hicho kwani kina tija kubwa katika jamii na uchumi wa kijani.

Naye Diana Obadia afisa kilimo, anawahamisha wakulima ambao hawajafanya maamuzi kuamua sasa kwani zao la mchikichi lina faida na hakuna kitu kinachotupwa, akizitaja miongoni mwa faida alisema ni mafuta ya kula, mise kwaajili ya kitengeneza sabuni, maganda ya mise hutumika kama kuni, shina hutumika kama mbao za kutengeneza vitanda na mvinyo pamoja na matawi ambayo hutumika katika ujenzi na kutengeneza fagio.

Kwa upande wa mkulima wa mchikichi Timotheo Rusulie kutoka kata ya Kagera manispaa ya Kigoma Ujiji alisema ameamua kuanza kulima zao hilo baada ya kuapata mafunzo kutoka TARI mwaka 2019 na mpaka sasa ameshashapanda miche 230 sawa na hekta nne za miche ya tenera anayoendelea kuihudumia kwa kufuata kanunui za kilimo huku dhima yake ikiwa kupanda hekai 10 sawa na miche takribani 550.

Alisema ameng’oa miche ya zamani ya mawe au dura aliyoikuta ikiwa shambani kwa  kuamini ina zaidi ya miaka 60 shamabani ili kupata nafasi zaidi ya kupanda miche ya kisasa anayokiri kuwa itamuingizia kipato zaidi akilinganisha na miche ya zamani na kuishukuru serikali kwa kubuni mpango huo kwa lengo la kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja sambamba na kuondoa changamoto za ajira kwa vijana wenye nia ya kufanikiwa kwa njia halali za kutajiingizia kipato.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma