skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Lusungu Helela

Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kushirikiana na Serikali ya Azerbaijan kubadilishana uzoefu katika utoaji wa huduma bora na ya pamoja ‘‘One Stop Service Center” kwa wananchi kufuatia nchi hiyo kupiga hatua kubwa katika eneo hilo.

Imeelezwa kuwa tangu nchi hiyo ilipoanza kutoa huduma hiyo ya pamoja kwa wananchi wake imesaidia tatizo la rushwa kuisha kabisa kwani uwezekano wa kuonana ana kwa ana kati ya wananchi na watoa huduma umepungua kwa kiasi kikubwa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene mara baada ya kufanya mazungumzo na timu ya wataalamu ya Wakala wa Taifa kwa Utumishi wa Umma na Ubunifu wa Kijamii ya nchini Azerbaijan jijini Dar es Salaam.

“Mimi pamoja na wataalamu kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali tumefanya mazungumzo na timu ya wataalamu kutoka nchini Azerbaijan ambapo wametueleza jinsi walivyofanikiwa katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi wao ambapo na sisi tumewaelezea jinsi tunavyofanya maboresho mbalimbali katika eneo hilo’’ amesema Mhe. Simbachawene

Waziri Simbachawene (katikati) katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Azerbaijan

Amefafanua kuwa  Serikali imejipanga kuanzisha vituo 31 vya  utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia dirisha moja ambapo kwa kuanza kila mkoa utakuwa na kituo kimoja huku Jiji la Dar es Salam kutokana  na uwingi wa watu litakuwa na vituo vitatu na Zanzibar kutakuwa na vituo viwili.

Amesema lengo la vituo hivyo ni kuhakikikisha Wananchi wanapata huduma za Serikali katika eneo moja hali itakayosaidia kupunguza mianya ya rushwa pamoja na ukiritimba.

‘‘Tunaamini kupitia kikao hiki cha kubadilishana uzoefu na wenzetu wa Azerbaijan, tutaboresha huduma zetu na wananchi watazifurahia’’ amesema Mhe. Simbachawene.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wakala wa Taifa kwa Utumishi wa Umma na Ubunifu wa Kijamii ya nchini Azerbaijan, Mhe. Ulvi Mehdiyevamesema nchi yao iko tayari kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha mifumo ya kidijitali inatumika katika utoaji huduma ya pamoja kwa wananchi kwa lengo la kuokoa muda wanaoupoteza katika kupata huduma za Serikali.

Mwenyekiti huyo, Ulvi Mehdiyev, amesema Tanzania ikianza kuutekeleza mfumo huo, tatizo la rushwa litaisha katika ofisi za Serikali, uzalishaji utaongezeka kwani wananchi watakuwa na muda mrefu wa kuzalisha badala ya kutumia muda huo kuzunguka kufuatilia huduma katika ofisi za Serikali pamoja na kasi ya wananchi kulipa kodi itaongezeka kufuatia huduma bora watakazozipata Serikalini.

Ujio wa Wataalamu hao kutoka nchini Azerbaijan ni matunda ya ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Mpango aliyoifanya mwezi Machi mwaka huu nchini humo.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma