skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Mwandishi Wetu, MoHA, Geneva.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni anatarajia kuiwakilisha Serikali ya Tanzania katika Kikao cha 73 cha Kamati Tendaji ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wakimbizi (UNHCR).

Kikao hicho ambacho kinaanza leo Jumatatu Oktoba 10, 2022, kitafanyika katika jijini la Geneva, nchini Uswisi, Ulaya Magharibi kitajadili masuala mbalimbali yakiwemo jinsi ya kuwahifadhi na kuwasimamia Wakimbizi waliopo katika nchi mbalimbali duniani.

Waziri Masauni ameambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi wa Wizara hiyo, Sudi Mwakibasi tayari wamewasili jijini Geneva nchini hapa, Jumapili Oktoba 9, 2022, akiwa tayari kuiwakilishi Tanzania katika Kikao hicho kwa kutoa taarifa ya Wakimbizi waliopo nchini.

Masauni na wasaidizi wake wamepokelewa na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania nchini Uswisi, Maimuna Tarishi, Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu Tanzania, Hoyce Temu na Maafisa mbalimbali wa Ubalozi huo na baadaye kufanya kikao na maafisa hao wa ubalozi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (katikati) akizungumza katika kikao na Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Uswisi wakati alipowasili katika jijini la Geneva nchini humo jana Oktoba 9, 2022 kwa ajili ya kuiwakilisha Serikali katika Kikao cha 73 cha Kamati Tendaji ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wakimbizi (UNHCR).

Akizungumza katika kikao hicho cha mapokezi kilichofanyika ofisi za ubalozi huo, jijini humo, amemshukuru Balozi Tarishi pamoja na maafisa wake kwa mapokezi mazuri na ameomba ushirikiano nao zaidi mpaka kikao hicho cha siku tano kitapomalizika.

“Mheshimiwa Balozi pamoja na maafisa wote wa ubalozi huu, nawashukuru sana kwa mapokezi mlionipa, nashukuru kwa miongozo mbalimbali kuhusu kikao hicho, naamini tutakuwa pamoja katika kuiwakilisha Serikali katika siku zote za kikao,” alisema Masauni.

Awali Balozi Tarishi alishukuru kwa Waziri pamoja na msafara wake kwa kuwasili salama nchini humu na watakuwa pamoja naye katika kikao hicho muhimu ambacho kinatarjia kutoa dira kuhusu kuwahudumia wakimbizi.

Mkurugenzi wa idara ya huduma kwa wakimbizi wa Wizara ya mambo ya ndani Bw. Sudi Mwakibasi. Picha zote kwa hisani ya Michuzi Blog

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwakibasi alisema Tanzania imekuwa mjumbe wa muhimu kwenye Kamati Tendaji ya UNHCR kufuatia historia ya muda mrefu kwenye uhifadhi na usimamizi wa masuala ya Wakimbizi nchini Tanzania.

“Mheshimiwa Waziri, kikao hiki ni Kikao kazi ambacho hufanyika kwa mujibu wa ratiba kikiwa na lengo la kujadili masuala mbalimbali ya Wakimbizi ambapo Tanzania pia ni moja ya nchi duniani inayohifadhi na kusimamia wakimbizi,” alisema Mwakibasi.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma