Taasisi ya vyombo vya habari kusini mwa Afrika inaadhimisha miaka 30 tangu kuasisiwa huku kukiwa…
Na. Mwandishi wetu
Tanzania imeahidi kuendelea kuwapokea wahamiaji na waomba hifadhi ambao watakidhi vigezo kutokana na sheria za uhamiaji, sheria za Ukimbizi na sheria za usalama wa nchi
Hayo yamebainishwa kwa nyakati tofauti na Waziri wa mambo ya Ndani ya nchi Mhandisi Hamad Masauni wakati alipotembelea mkoa wa Kigoma na kugagua vituo vinavyotumika kuwapokea, kuwahakiki na kuwasajili waomba hifadhi kutoka jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanaotaja kuikimbia nchi yao kutokana na hali duni ya usalama
Mhe. Masauni alisisitiza kuwa waomba hifadhi wote wanaoingia nchini Tanzania watahojiwa na kuhakikiwa ili kubaini uhalali wa sababu zinazopelekea kuzihama nchi zao na kuingia nchini Tanzania na kuhakikisha wasiostahili kupewa hifadhi wanabainika na kuchukuliwa hatua

“Tanzania imekuwa na historia nzuri ya kuwapokea raia wa nchi nyingine ambao wanakuja kuomba hifadhi, hivyo tutawapa hifadhi wale watakaostahili na wasio stahili watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria zetu, hatuwezi kuruhusu watu walioingia kinyume cha sheria na kuishi Nyarugusu au katika vijiji watumia fursa ya kuomba hifadhi kuhalalisha makosa yao, tukiwabaini tutawachukulia hatua” alisisitiza Masauni
Waziri Masauni alitembelea pia kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu ambayo inatumika kuhifadhi wakimbizi kutoka Jamhuri ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo sambamba na waomba hifadhi wapya kutoka DRC ambao wanaendelea kuhojiwa ili kuwapa uhalali wa kuwa wakimbizi.

Zaidi ya waomba hifadhi wapya 6000 wamekwishapokelewa mkkoani Kigoma tangu March 5 mwaka huu wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.