skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Adela Madyane – Kigoma

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoani Kigoma imeeleza kufanikiwa kuokoa zaidi ya milioni 12 baada ya kufanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo 27 yenye thamamani ya zaidi ya bilioni nane uliofanyika katika kipindi Aprili hadi Juni 2022.

Akisoma taarifa hiyo kwa waandishi wa habari John Mgallah, naibu mkuu wa TAKUKURU mkoani humo amesema wameokoa pesa hizo baada ya kufanya ufuatiliaji wa manunuzi na kubaini kuwepo kwa ukiukaji wa taratibu za mkataba wa manunuzi uliopelekea kununuliwa kwa vifaa chini ya viwango.

“Tulifanya ufuatiliaji katika wilaya ya Kasulu na kubaini baadhi ya vifaa vilivyonunuliwa vyenye thamani ya milioni tatu havijakidhi masharti ya manunuzi, na wilaya ya Buhigwe tulibaini uwepo wa vifaa vya ujenzi vyenye vipimo visivyokidhi makubaliano vyenye thamani ya milioni 9, zabuni zilisitishwa na kuletwa vifaa kulingana na masharti ya mkataba na hivyo kuokoa pesa hizo” Amesema Mgallah

Naibu mkuu wa TAKUKURU mkoani Kigoma Akitoa tarifa ya miezi mitatu ya utekelezaji wa majukumu yake.

Amesema fedha za miradi ya maendele ni za wananchi na hivyo watahakikisha wanabaini mapungufu katika miradi hiyo ili kupata miradi bora yenye kukidhi thamani ya fedha.

Sambamba na ufuatiliaji wa miradi taasisi hiyo imepokea malalamiko 96 yaliyofanyiwa uchunguzi na kubainika kuwa kati ya malalamiko hayo 76 yalihusu rushwa na sekta inayoongoza kwa malalamiko kuwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) ambapo jumla ya malalmiko 46 yaliwasilishwa.

Hata hivyo TAKUKURU mkoani Kigoma imeweza kuwafikia wananchi zaidi ya 2288 walionufaika na elimu ya namna ya kushiriki katika kupambana na rushwa zilizofanyika kayika semina, mikutano ya hadhara, katika klabu za wapinga rushwa, kwenye maonesho na redioni.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma