skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Ajiunga upya na shule na sasa ni mhandisi mtarajiwa wa umeme wa majumbani

Na. Adela Madyane

MAKUZI, UJAUZITO NA KUFUKUZWA SHULE

Akiwa na miaka mitano Leticia Patric (21) mkazi wa kata ya Katubuka manispaa ya Kigoma Ujiji anakutana na changamoto ya kufiwa na wazazi wake, na kulelewa na  shangazi yake  mpaka alipopata ujauzito usiotarajiwa akiwa kidato cha tatu na kubadili ndoto zake za kuwa mwalimu hadi kuwa mke wa mtu na mama wa nyumbani na sasa ni mama wa watoto wawili ambao licha ya kuwapenda lakini haishi kuiwaza ndoto yake ya tangu utoto wake (Ualimu).

Leticia anadai ujauzito wa kwanza aliupata mnamo mwaka 2018 akiwa na umri wa miaka 17 baada ya kufukuzwa nyumbani kwa shangazi yake usiku wa manane na kuhifadhiwa na majirani ambapo anakutana na mwanaume ambaye baada ya kumsaidia na kuishi naye kama mke alimpatia ujauzito na kisha kumtelekeza bila matunzo yoyote.

Baada ya kujifungua mtoto wake wa kwanza mnamo April 2019 alirudi kwa shangazi yake ambaye aliendelea kumlea kwa kuogopa macho ya watu, lakini kwa sababu ya manyanyaso aliyoyapata alifanya maamuzi ya kuolewa tena mtoto wake akiwa na miezi tisa, ambapo alidumu kwa mwaka mmoja na kufukuzwa tena akiwa na ujauzito wa mtoto wake wa pili huku hali yake ya maisha ikizidi kuwa mbaya.

Leticia anadai kuwa changamoto iliyomfanya apate ujauzito katika umri mdogo  ni manyanyaso aliyokuwa akiyapata kutoka kwa shangazi yake  pamoja na mtoto wake aliyekuwa akitaka kumbaka na kuwa chanzo kikubwa cha yeye kufukuzwa pale nyumbani, na kuwa pamoja na changamoto zote shangazi yake  alikataa asilelewe na ndugu mwingine mpaka pale watakapomlipa pesa alizotumia kumuhudumia toka alipokuwa mtoto mpaka umri aliofikia jambo ambalo lilikuwa gumu kwani ndugu hawakuwa na pesa ya kumlipa shangazi yake.

“Mtoto wa shangazi alitaka kunibaka shangazi alipokuwa kwenye shughuli zake, nilikataa huku nikipiga kelele za kuomba msaada kwa majirani, lakini shangazi aliporudi nyumbani usiku alinifukuza kwa madai kuwa namsemea uongo mtoto wake ambaye ni binamu yangu na kunitaka niondoke kabisa nyumbani kwake na nisiende kwa ndugu yoyote mpaka wamlipe pesa alizotumia kunilea,””Anasema Leticia

Leticia Patrick akizungumza na Buha FM na Buha TV alipotembelewa chuoni FDC Kihinga kusikiliza hadithi ya maisha yake

Anasimulia kuwa wakati anapata matatizo hayo mwaka 2018, alikuwa akisoma katika sekondari ya Katubuka iliyopo manispaa ya Kigoma Ujiji, akalazimika kutoroka shule kwa miezi miwili huku akiwa anashinda kwa shangazi yake kama hayupo na kurudi kuishi kwa jirani mara tu shangazi yake anaporejea nyumbani na baada ya kugundulika kuwa mjamzito mnamo Agosti mwaka huo aliamua kwenda kuishi kwa mwanaume aliyempa ujauzito akitarajia kuishi kwa furaha japo matarajio yake hayakutimia.

Leticia anasema alipata ujauzito huo kwa hila za mwanaume huyo ambaye alimuita nyumbani kwake akimtaka akaonane na dada yake, alipofika alimkuta akiwa na rafiki zake ambapo baadae alimuingilia kimwili na kupata ujazito amabao ulisababisha akafukuzwa shuleni na pia kufukuzwa na  mwanaume huyo aliyempa ujauzito, hakuwa na namna zaidi ya kurudi kwa shangazi yake japo mahitaji yake ya msingi na ya kutunza ujauzito aliyapata kwa siri kutoka kwa baba yake mdogo  huku ikimlazimu kufanya vibarua vya kufuma mashuka ili kujipatia kipato.

Changamoto ziliongezeka baada ya kujifungua kwakuwa niliugua sana na kukosa msaada, wazazi wa yule mwanume walikataa nisihudumiwe na mtoto wao kwa madai kuwa mtoto wao bado mdogo hawezi kumpa mwanamke ujauzito,  baada ya mwanangu kufikisha miezi tisa nilipata msamalia mwema ambaye alinichumbia na akakubali kunitibisha kisha anioe, na alikubali kunilea mimi pamoja na mwanangu, na ndipo nilipofanya maamuzi ya kuolewa tena mwaka 2019, japo nilifukuzwa pia baada ya kukaa naye kwa mwaka mmoja kwakuwa mama yake hakupenda mwanae aoe mwanamke mwenye mtoto” Anasema Leticia

Baada ya kukaa kwenye mahusiano kwa kipindi hicho, Leticia alipata ujauzito wa pili ambapo shida kama za awali ziliibuka tena na kumuacha akiwa hana mbele wala nyuma kwani mara baada ya ujauzito mwanume huyo alimchukia na kumtelekeza yeye na mwanae pamoja na ujauzito na kumfanya amtegemee baba mkwe wake ambaye alijitahidi kumuhudumia kadri alivyoweza mpaka alipofariki na kumuacha akiwa hajui afanye nini.

“Tamaduni za familia hii mwanamke akiolewa anakuwa kama binti wa kazi, mila ambayo ilipigwa vita na baba mkwe, baada ya kufariki ile tamaduni iliendelea na kunifanya nichoke sana, nilivumilia ili nijifungue ila haikuwezekana kwa kuwa Agosti 2021 alinifukuza saa mbili za usiku,” anasema.

“Alitoa nguo zangu nje, nilipojaribu kuomba msaada kwa mama yake na ndugu zake wengine walinitukana sana nikaamua kurudi kwa babu yangu kwa ajili ya kunilea kwa kuwa kwa shangazi niliapa kuwa sitarudi tena,” anasema Leticia.

Hata hivyo Leticia alishindwa kumudu maisha yake, pamoja na kufanya shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato bado hazikuweza kukidhi mahitaji yake wala ya watoto wake, aliamua kurudi kwa shangazi yake na kuomba amuwezeshe kitu cha kufanya ili aweze kukidhi mahitaji yake kwani babu yake ni mzee anayehitaji msaada, ndugu zake wengine waliogopa kumsaidia kwa sababu shangazi yake angeshinikiza alipwe fedha, japo hakufanikiwa na ndipo aliponyang’anywa watoto wake na wanaume aliozaa nao na kumuacha akiishi peke yake akipamana kwaajili ya mustakabali wa maisha yake.

Katika harakati za kujikwamua kiuchumi Leticia anakutana na Muuguzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa Kigoma, Maweni akamwambia kuna nafasi ya elimu na mafunzo kwa watoto wa kike katika chuo cha maendeleo ya wananchi (FDC) Kihinga, na ni baada ya kumuona kuwa bado mtoto mdogo ambaye anaweza kutimiza ndoto zake pamoja na changamtoto alizokutana nazo

Muuguzi huyo anamwambia kuwa mafunzo yanatolewa bure kwa wasichana waliozaa wakiwa shuleni kabla ya kufanya mtihani wa kidato cha nne na serikali inalipia kila kitu na  mtu huamua kukaa bweni au kutwa na ndipo Leticia alipohamasika na kufika chuoni  hapo na kuambiwa anunue sare, godoro, vyombo vya chakula na ndoo ambapo alimuomba baba yake mdogo akampa pesa ya kununua vifaa na kuanza shule mwezi April 2023.

LETICIA ANAANZA MASOMO YAKE KATIKA PROGRAMU YA ELIMU HAINA MWISHO

Leticia anaanza upya safari yake ya elimu ili kutimiza ndoto yake baada ya ramani yake kupindishwa kwa miaka mitano, akiwa na mwezi mmoja tu shuleni hapo, kwa sasa anasoma kozi ya umeme majumbani sambamba na elimu ya sekondari kwa miaka miwili akiwa mwaka wa kwanza kwa kidato cha kwanza na cha pili anasisitiza kuwa amejipanga kusoma kwa bidii na kuwa mwalimu wa sekondari, kwani ameshapata mwanga mpya na namna ya kutimiza ndoto zake.

Anaishukuru serikali kwa program hiyo muhimu kwa watoto wa kike wenye nia ya kurejea kwenye ndoto zao maana hakutegemea kama angekuja kusoma tena na anaiomba serikali iwaendeleze zaidi na kuwasaidia namna ya kuwalea watoto nyumbani hasa wanaoishi kwenye mazingira magumu ili wawe na uhakika wa kusoma na kupata ufaulu mzuri na kuwaasa wasichana waliopo mashuleni kuaacha tamaa ya kupata vitu vizuri kabla ya wakati.

Leticia (katikati) akiwa katika karakana ya umeme kwa ajili ya mafunzo katika chuo cha maendeleo ya jamii Kihonga mjini Kigoma

WASICHANA WENGINE KATIKA CHUO CHA FDC WALIOPO KWENYE MPANO WA ELIMU HAINA MWISHO.

Katika chuo cha FDC Kihinga, Leticia hayupo peke yake, yupo pia Luciana Bagabo aliyepata ujauzito akiwa kidato cha nne mwaka 2019 baada ya kurubuniwa na rafiki yake aliyekuwa anamsaidia kupata chakula wakati mama yake anaumwa na kukaa hospitali ya Muhimbili kwa zaidi ya mwaka mmoja na alipomtaka kimapenzi alikubali kwa kuwa alimuona anamfaa ila baada ya kupata ujauzito alimtelekeza akabaki analelewa na bibi yake.

Luciana alisikia matangazo ya kurudi shuleni kwa watoto wa kike kupitia redio ya kijamii na kuamua kurudi ili kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari na sasa yupo mwaka wa pili na anatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu mwaka huu 2023 na yeye anachukua kozi ya umeme wa majumbani itakayomsaidia kupata pesa wakati anasubiri matokeo

Naye Grace Gasper (18) kutoka mkoa wa Geita baada ya kupata ujauzito akiwa kidato cha kwanza Agosti 2019 aliitwa Kigoma kufanya kazi kwa mama yake mkubwa ili kuficha aibu ya nyumbani kwao, baada ya mtoto kukua aliamua kurudi shule ili kujiendeleza na kupata mwanga wa kuzifikia ndoto zake.

MAAFISA KUTOKA FDC KIHINGA

Akizungumzia jambo hilo, Prisca Kalima mratibu wa mafunzo ya mpango wa elimu haina mwisho Kihinga FDC kwa kushirikiana na wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi anasema mfumo huo umesaidia kurejeshwa ndoto za mabinti zilizopindishwa na kwamba changamoto iliyopo ni muitikio mdogo wa jamii kwani wanaojitokeza ni wachache wanaojitokeza ni wachache ukilinganisha na changamoto iliyopo katika jamii

Naye Henry Lyioba anasema masomo ya sekondari ya elimu haina mwishokwa mara ya kwanza yalianza mwaka 2020 katika chuo hicho na walianza wakiwa na wanafunzi 53 ambao kati yao 36 walifanya mtihani wa kidato cha nne.

 Anasema mwaka 2021 walisajiliwa watoto 75 ambao kati yao waliofanya mtihani walikuwa watotot 14 pekee huku chanzo cha tatizo hilo kuwa baadhi ya wanafunzi kuamini katika kozi za ufundi walizochukua na kuamua kuachana na elimu ya sekondari  kwa kuhisi kozi walizopata zitawasaidia kuingiza kipato kwa haraka na kuanza kuendeleza maisha yao.

Anasema mpaka sasa chuo kina jumla ya wanafunzi 320 huku walio katika mpango wa elimu haina mwisho kuwa wanafunzi 86 na kwamba  uwezo wa shule ni kumudu wanafunzi 100 na kuiomba serikali kuwapatia walimu kwani kwasasa mpango wa elimu haina mwisho unatumia walimu wa ziada na kwamba wanahitaji walimu sita ili waweze kuondoa upungufu uliopo na kutoa elimu inayostahiki.

WANAFUNZI WALOPATA UJAUZITO NA KURUDI KUSOMA KATIKA MFUMO RASMI.

Katika mfumo rasmi gazeti la Nipashe linakutana na Monica Peter mwanafunzi wa kidato cha tano katika sekondari ya Buronge akichukua mchepuo wa HGK anasema alipata changamoto ya ujauzito 2020, akiwa anaelekea kufanya mtihani wa kidato cha nne, alifanya mtihani na kupata daraja la tatu na kukaa nyumbani mwaka mzima baadae ili kumlea mtoto wake.

Anasema sasa mtoto wake ana mwaka mmoja na miezi tisa, akiwa mwenye afya njema na maendeleo mazuri, anasema mazingira ya shule ni mazuri na hakuna unyanyasaji wa aina yoyote na hivyo itakuwa rahisi kwake kufikia ndoto yake ya kuwa mwanasheria

Naye Brandina Muhungu anasema alipata ujauzito akiwa kidato cha nne na kupata daraja la tatu lililomuwezesha kuingia kidato cha tano kwa mchepuo wa HGK, baada ya kujifungua familia yake ilimuwezesha kurudi shuleni huku watoto wake mapacha wakilelewa na mama yake mzazi.

MAONI YA WADAU WA ELIMU NA USHAURI WA WAZAZI.

Akiliongelea hilo mwalimu mkuu msaidizi sekondari Buronge, Lazaro Bukuku yenye wavulana 800 na wasichana 702 anasema mpango huu ni bora kwasababu umeondoa mapungufu na kurejeshwa haki iliyoponywa kwa watoto wa kike na kwamba katika shule hiyo wapo watoto wawili wote wa kidato cha tano huku changamoto kubwa inayowasibu kuwa kuuguliwa kwa watoto wao.

Grace Muhoza mzazi wa Brandina, anawashauri wazazi wasiwazuie watoto wao kurudi shule, waondoe chuki na hasira, wawatie moyo na kuwasamehe ili waendelee mbele na elimu kwani hawajui kesho yao huenda ndio watakaokuwa faraja ya familia na kwamba walimu wanapaswa kuendelee kuwatia moyo na kuwajengea uwezo wa kufanya vizuri zaid.

Afisa elimu Paulina Ndigeza, anadai takwimu za ujauzito zimepungua kwa mwaka 2020 -2022 kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha sita kutoka mimba 32 kwa mwaka 2020 mpaka sita kwa mwaka 2022 na kwamba hayo ni matokeo ya vituo vya ushauri nasaha vilivyopo mashuleni kwajili ya kuwaelimisha watoto wakike.

Anasema baada ya kutolewa kwa waraka wa wanafunzi waliopata ujauzito kurudi shuleni wanafunzi 27 walirudi shuleni kwenye mpango rasmi.

Akifafanua zaidi anasema wameweza kurudisha wanafunzi 363 wa sekondari wanaosoma nje ya mfumo rasmi katika vituo vilivyotengwa na serikali ambapo kati ya hivyo ni Kihinga FDC yenye wanafunzi 86 na wanaendelea vizuri chini ya uangalizi wa idara ya elimu.

Kwa upande wa shule za msingi Ndigeza anasema zipo jitihada mbalimbali zilizofanyika kuinua elimu ikiwemo kurejesha wanafunzi 500 waliofeli mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2022 ili waweze kufanya mtihani mnamo mwezi October 2023.

Ameongeza kuwa wameweza pia kurejesha wanafunzi wa 360 waliocha shule kwa sababu za utoro ambao pia watafanya mtihani mwaka huu.

Amebainisha kuwa mpaka sasa wapo wanafunzi 1223 waliopata changamoto mbalimbali na kuacha shule wanaojifunza kupitia mfumo rasmi wenye vituo 16 vinavyopatikana katika kila halmashauri zote za mkoa wa Kigoma na nje ya mfumo rasmi katika vituo tisa ikiwemo FDC Kihinga na Malagarasi.

Ndigeza ametaja ujauzito na utoro kuwa unasababishwa na masoko ya usiku na shughuli za uvuvi kwa lengo la kujipatia kipato.

Chuo cha FDC Kihinga kinatoa kozi za umeme majumbani, useremala, uungali vyuma, mabomba, kilimo na umemewa mashine kozi ambazo zinamsadia mwananfunzi kuwa na ujuzi utakaomsaidia kuingiza kipato cha halali.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma