skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki,Simiyu

Wananchi mkoani Simiyu wamesema wamepata fursa za kujifunza dalili na namna ya kupata tiba ya ugonjwa wa kifua kikuu kupitia elimu ambayo imetolewa wakati wa maonesho yaliyoandaliwa kwa ajili ya maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani ambayo yamefanyika kitaifa mkoani hapo.

Wananchi hao wamesema hayo kwa nyakati tofauti wakiwa kwenye maadhimisho hayo huku wakiongeza kuwa kwa Sasa wanaweza kutambua namna ugonjwa huo unavyoambukizwa na namna ya kujikinga nao.

“Tumefika kwenye mabanda mengi yaliyopo kwenye viwanja hivi tumepata elimu ya namna ya kujikinga tumechunguzwa na waliobainika wamepata ushauri na kuanza matibabu tunashukuru serikali yetu kwa kuleta maadhimisho hayo kwetu mikoa ni mingi lakini wetu umependelewa” amesema Masanja Kwilasa.

Awali akitoa salamu za mkoa wa Simiyu mkuu wa mkoa huo Dkt Yahaya Nawanda amesema mkoa huo umepokea mashine nane za kupima vinasaba vya vimelea vya kifua kikuu na kwamba vifaa hivyo vitakuwa chachu mhimu katika mapambano na udhibiti wa ugonjwa huo.

Dkt Yahya Nawanda mkuu wa mkoa wa Simiyu

Kwa upande wake waziri ya afya Ummy Mwalimu amesema watu 25,800 nchini wanapoteza maisha kwa mwaka kutokana na kifua kikuu sawa na watu 71 kwa siku huku akiongeza kuwa serikali imejitahidi kuhakikisha vipimo na dawa zinapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini.

Kwa upande wake Waziri Mkuu amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 duniani zenye maambukizi makubwa ya kifua kikuu ambazo kwa pamoja zinachangia asilimia 87 ya wagonjwa wote duniani.

Serikali kwa kushirikiana na wadau nchini iliweza kutumia wahudumu wa afya ngazi za jamii wapatao 3600 kutoa elimu kwa wamiliki wa maduka ya dawa muhimu 1440 na waganga wa tiba asili 900 ili waweze kutoa elimu na vifaa kwa wahisiwa wa kifua kikuu ili waende kwenye vituo vya kutolea huduma.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa akiwahutubia watanzania kupitia jamii ya mkowa wa Simiyu

Maadhimisho hayo yameenda sambamba na kauli mbiu isemayo “Kwa pamoja tunaweza kutokomeza kifua kikuu Tanzania.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma