skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Anita Balingilaki, Simiyu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe, Kassimu Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani ambapo kitaifa yatafanyika mkoani Simiyu.

Hayo yamesemwa na mganga mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt Boniface Marwa wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mkoani hapo huku akiongeza kuwa kilele cha maadhimisho hayo ni Marchi 24,2023 kwenye viwanja vya halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani hapo.

Dkt Marwa amesema maadhimisho hayo ni fursa kubwa mkoani hapo kwani yataweza kufungua ufahamu na uelewa kwa wananchi kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu.

Amesema tayari maandalizi yameanza kuelekea maadhimisho hayo ambapo huduma mbalimbali zinaendelea kutolewa ikiwemo upimaji na lipo gari maalum lenye vifaa vyote vinayotumika kwenye utambuzi wa kifua kikuu.

“Gari hili litazunguka katika maeneo mbalimbali ya halmashauri ya mji wa Bariadi pamoja na halmashauri jirani kufanya upimaji na kuibua wagonjwa wapya ambao wataanzishiwa dawa”amesema Dkt Marwa

Wataalam wa afya kutoka Wizara ya Afya ambao wamewasili mkoani Simiyu kwa maandalizi ya kitaifa

Kuhusu matibabu ya ugonjwa huu Dkt Marwa amesema ugonjwa huo unatibika, dawa zimeboreshwa na mgonjwa anatumia kwa muda wa miezi sita tofauti na awali ambapo mgonjwa alitakiwa kutumia dawa kwa kipindi cha zaidi ya miezi 11 huku akiongeza kuwa dawa hizo hazina madhara yoyote kwa watumiaji.

Dkt Marwa amesema ugonjwa huo ni hatari kama usipobainika mapema na kuanza matibabu kwani unaambukizwa kwa haraka kwa njia ya hewa na mgonjwa mmoja anaweza kuambukiza watu wengi katika familia yake na watu wengine ambao anachangamana nao katika shughuli mbalimbali ikiwemo za uzalishaji.

Baadhi waandishi wa habari waliohudhuria mkutano wa wanahabari na mganga mkuu wa mkoa wa Simiyu

Dkt Marwa amesema kati ya wagonjwa wanaowabaini chini ya asilimia 20 wanaupungufu wa kinga mwilini na zaidi ya asilimia 70 ni wagonjwa ambao hawana maambukizi ya virusi vya ukimwi wala hawana upungufu wa kinga mwilini.

“Jamii iachane na mtazamo eti ugonjwa huu wa kifua kikuu unawapata zaidi wagonjwa ambao wameathirika na virusi vya ukimwi /wana upungufu wa kinga za mwilini unaotokana na magonjwa ikiwemo saratani, katika ugunduzi na utambuzi wa wagonjwa tumebaini sio hao tu katika wagonjwa wote tunaowabaini wanaokuwa na upungufu wa kinga mwili na virusi vya ukimwi ni chini ya asilimia 20, wananchi waache dhana potofu mtu yeyote hata kama ana kinga thabiti bado anaweza akapata maambukizi, anaweza kuwaambukiza wengine hivyo kila mmoja achukue tahadhari”amesema Dkt Marwa.

Dkt Marwa amesema tahadhari zinazotakiwa ni pamoja na kukaa katika maeneo ambayo Yana mzunguko mzuri wa hewa kutojazana sehemu moja, kujenga nyumba zenye madirisha makubwa yanayopitisha hewa na kutolala watu wengi ndani ya chumba kimoja.

Aidha amesema ugonjwa huo uwapata watu wa rika zote wakiwemo watoto wadogo ambao wengi wao wengi wao uwa na utapiamlo na matatizo mengine ya kiafya.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma