skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki, Bariadi 

Wananchi wa kijiji cha Nyanguge kilichopo kata ya Ngulyati  wilayani Bariadi mkoani Simiyu wanatarajia kuondokana na kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 10 kufuata huduma ya afya kwenye zahanati ya Nyamswa iliyopo kijiji cha Nyamswa kata ya Gambosi baada ya kuamua kutumia nguvu zao kujenga zahanati katika eneo lao.

Hayo yamesemwa na afisa mtendaji wa kijiji cha Nyanguge George Mtengera wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa zahanati hiyo mbele ya mkuu wa wilaya ya Bariadi Simon Simalenga ambaye alizuru katika kijiji hicho kukagua shughuli za maendeleo na kushuhudia mwamko wa wananchi katk=ika kuchangia shughuli za maendeleo. 

Ujenzi huo ulianza mwaka 2016 ukiwa chini ya usimamizi wa uongozi wa kijiji na michango ya wananchi na ofisi ya mbunge wa jimbo hilo imetumika mpaka kwenye lenta na kisha serikali kuu kuunga mkono nguvu za wananchi kwenye zoezi la ukamilishaji.

Jumla ya kiasi cha shilingi milioni 31,603,250 zilikusanywa na kati ya fedha hizo ofisi ya mbunge ilichangia bati 230 sawa na kiasi cha shilingi milioni 8,970,000 na kiasi kilichobaki kikiwa nguvu za wananchi.

“Mwaka wa fedha 2021/22 serikali kuu kupitia halmashauri ya wilaya ya Bariadi tumepokea kiasi cha shilingi milioni 50,000,000 kwaajili ya ukamilishaji wa zahanati ya Nyanguge” amesema Mtengera.

Mkuu wa wilaya ya Bariadi ndugu Simon Simalenga (mwenye shati la maua) akishiriki shughuli ya ujenzi wa Zahanati kwa kufyatua matofali, Picha. na Anita Balingilaki

Mtengera amesema zahanati hiyo unatarajiwa kukamilika Mei 12,2023 na ujenzi wake unatekelezwa kwa mfumo wa “force account”  na mpaka April 18, 2023 jumla ya kiasi cha shilingi milioni 7,072,500 kimeshatumika kwaajili ya ununuzi wa vifaa huku kiasi cha shilingi milioni 42,927,500 bado kikiwa hakijatumika.

Mara baada ya kupokea taarifa hiyo, mkuu wa wilaya hiyo Simon Simalenga  aliwapongeza wananchi wa kijiji hicho huku akiongeza kuwa ni kijiji cha mfano wa kuigwa kwa ushiriki wa shughuli za maendeleo.

“Nataka niwatie moyo muendelee na moyo huo wa kujitolea sio tu kwenye eneo la ujenzi wa zahanati, jengeni maboma sisi (serikali) tutawashika mkono, serikali ya Dkt Samia inazo fedha za kutosha, nyie ni mashuhuda fedha nyingi zimeletwa kwenye miradi mingi ya maendeleo,  kama ni boma la nyumba ya mtumishi anzeni sisi tukija tunawapokea tunakamilisha” alisisitiza DC Simalenga.

Mbali na hayo mkuu wa wilaya ya Bariadi Simon Simalenga alitoa wito kwa akina baba kuwa sehemu ya kuwahimiza wake zao wenye ujauzito kuhudhuria kliniki ili mama atazamwe maendeleo ya mtoto wake hatua itakayopelekea kutohatarisha afya yake na mtoto/watoto walio tumboni.

Kijiji cha Nyanguge ni miongoni mwa vijiji vinne vilivyopo katika kata ya Ngulyati na kijiji hicho kinaundwa na vitongoji vinne ambavyo ni Madukani, Ng’hesha, Mwamola na Nyambuli.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma