skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mwandishi wetu, Dodoma

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amesema serikali imekuwa ikitekeleza mkakati wa kukuza ujuzi na kuwapatia stadi za kazi vijana kwa lengo la kuwezesha nguvu kazi kumudu ushindani katika soko la ajira.

Aidha, Mpango wa tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano hadi 2025, unalenga kuwafikia vijana 681,000 na tayari serikali imeanza makubaliano na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha mafunzo ya ujuzi na stadi yanatolewa kwa vijana.

Mhe.Katambi amebainisha hayo Aprili 24, 2023 bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum (CCM), Latifa Khamis Juakali aliyetaka kujua mkakati wa serikali wa kukuza ujuzi na stadi kwa vijana.

Akijibu swali hilo, Katambi amesema ili kukuza ujuzi na stadi za kazi kwa vijana, Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Kukuza Ujuzi wa Miaka 10 (2016/17 – 2025/26) ambao umelenga kuhakikisha nguvu kazi ya vijana kushiriki katika kujenga uchumi wa Taifa.

Ameeleza mkakati huo unatekelezwa kupitia program na mipango mbalimbali ya kukuza ujuzi na stadi kwa vijana inayotekelezwa na wadau mbalimbali wakiwemo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Amesema baadhi ya programu na mipango hiyo ni pamoja Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inayotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambayo tangu kuanza kutekelezwa mwaka 2016/17 imetoa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi kwa jumla ya vijana 118,415.

“Pia Mpango wa Mafunzo na Uwezeshaji wa Vijana kushiriki kilimo unaotekelezwa na Wizara ya Kilimo unaojulikana kwa jina la Building Better Tomorrow (BBT),” amesema.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma