skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Issa Sabuni – REA

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imewezesha kuweka historia kwa kufadhili mradi wa umeme wa maji wa Ijangala kuingizwa kwenye gridi ya Taifa na kuwanufaisha zaidi ya wananchi 4,500 wa vijiji nane vya wilayani Makete.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Nishati Lutheran (DKK) Investment Ltd; inayomiliki Mradi wa Umeme unaotokana na chanzo cha maji wa Ijangala, Elikana Kitahenga, amesema tayari mchakato wa kuingizwa kwenye gridi umeanza rasmi baada ya kukamilika ujenzi wa kituo hicho.

Mradi wa Umeme unaotokana na chanzo cha maji wa Ijangala kwa sasa una uwezo wa kuzalisha KiloWati 360 ambapo kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa maana yake ni kuwa kampuni ya Nishati Lutherani (DKK) Investment Ltd itaanza kuuza umeme huo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Akiongea na Wanahabari; Kitahenga amesema REA imetoa zaidi ya millioni 900 kwa awamu tatu katika kufadhili ujenzi wa mradi huo.

Amesema kukamilika kwa hatua hii ya kuanza kuingia Mradi wa Ijangala kwenye Gridi ya Taifa; kumetokana na uwezeshaji wa REA ambapo mwaka 2013, Mradi huo ulipokea awamu ya kwanza, shilingi milioni 133 na baadae mwaka 2016 Mradi ulipokea shilingi milioni 426 na awamu ya tatu, wanatarajia kupokea shilingi milioni 437.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Nishati Lutheran (DKK) Investment Ltd, Elikana Kitahenga (kulia) akimskiliza Mshauri Elekezi wa Mradi huo wa Ijangala, Prof. Zakaria Katambala kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) namna mashine za kuzalisha umeme zinazofanya kazi. Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umewezesha zaidi ya Mil900 kwa ajili ya ununuzi wa mashine za kufua umeme ambapo jitihada hizo zimewezesha umeme huo kuingizwa katika gridi ya taifa. (Picha na REA)

Amesema mradi huo ni ukombozi kwa wananchi wa vijiji vya Masisiwe, Tandala, Ikonda, Usagatikwa na Ihela kwa kupata umeme wa uhakika unaotokana na Mradi wa chanzo cha maji wa Ijangala.

Akieleza kuhusu tukio la kuingiza umeme kwenye Gridi ya Taifa; Mshauri Elekezi wa Mradi huo wa Ijangala Prof. Zakaria Katambala kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) amesema kazi imefanywa vizuri na Wakandarasi wanne na kuongeza kuwa zoezi la kuunganisha Kituo hicho na Gridi ya Taifa litakamilika ndani ya wiki moja.

Amezitaja kazi zilizofanywa na Wakandarasi hao wanne, kuwa ni pamoja na ujenzi wa bwawa linalokinga maji kutoka juu kuja chini ulipo Mradi (Power House); kazi nyingine ni ujenzi wa bomba la kusafirisha maji (Penstock) kutoka juu kuja chini kwenye mtambo wa kufua na kuzalisha umeme; kazi ya tatu ni ujenzi wa sehemu ya kuzalisha umeme (Power House) na sehemu ya mwisho ni ujenzi wa mfumo wa kuunganisha mtambo wa umeme wa chanzo cha maji ili uungane na umeme wa TANESCO.

“Kazi imefanyika vizuri, na Wawakilishi wa TANESCO wapo eneo la Mradi ili kuangalia ubora wa kazi yetu na kujiridhisha, waturuhusu kuanza kuingiza umeme unaozalishwa hapa kuingia kwenye Gridi ya Taifa”. Alisema Profesa Katambala.

Aidha, Kitahenga ameeleza zaidi kuws zoezi hilo linatarajia kushirikisha Wataalam kutoka REA, TANESCO na Mkandarasi aliyejenga njia ya umeme kuja kwenye chanzo cha kuzalisha umeme cha Ijangala; kampuni ya SILO Power na kuongeza kuwa linatarajia kuendelea kwa wiki mbili hadi tatu.

Picha inaonesha maporomoko ya mto kagera katika eneo la Rusumo wilayani Ngara, ni moja ya maporomoko mhimu ambayo yanajengwa kwa ajili ya kuzalisha umeme utakaoingizwa katika grid ya mataifa ya Burundi, Rwanda na Tanzania. picha na. Prosper Kwigize
Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma