skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Mwandishi wetu, Lilongwe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara hususan mpakani mwa Tanzania na Malawi ili wananchi waweze kunufaika na biashara zao.

Rais Samia ameyasema hayo kabla ya kuhitimisha ziara yake ya Kiserikali ya siku 3 nchini Malawi, ambapo pia amehudhuria sherehe za miaka 59 ya uhuru wa nchi hiyo.

Kwa pamoja, Rais Samia na Rais wa Malawi Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera wamewataka mawaziri husika kukaa chini na kutafakari namna ya kuondoa vikwazo  vya kibiashara ili maono ya Serikali zote mbili yaweze kufikiwa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kushoto mbele) akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ziara yake nchini Malawi kwenye Mkutano uliofanyika Blantyre nchini humo tarehe 7 Julai, 2023.

Rais Samia pia ameshuhudia utiaji saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya Tanzania na Malawi kuhusiana na mashirikiano kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Katika mkataba huo, upande wa Tanzania ulisainiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye pamoja na Waziri wa Habari na TEHAMA wa Malawi Mhe. Moses Kunkuyu Kalongashwa.

Vile vile Rais Samia ameipongeza Malawi kwa kuanza kufundisha somo la Kiswahili katika shule zake na kusisitiza kwamba lugha hiyo ndio itakayowaunganisha Waafrika.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ametembelea eneo la Kapeni view point Blantyre na kujionea athari zilizotokana na kimbunga Freddy ambapo watu wengi walipoteza maisha, mali na makazi.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma