Asema hadi sasa imeshawekeza dola za Marekani bilioni 10 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi…
Na. Mwandishi wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania itaendelea kuweka miundombinu ya kukuza biashara na Rwanda ili kuinua kiwango cha biashara kilichopo na kukuza uchumi wa nchi zote mbili.
Rais Samia amesema hayo leo wakati yeye pamoja na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame wakizungumza na vyombo vya habari Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Rais Samia amesema kulingana na uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Rwanda kiwango cha biashara kilichopo hakiendani na rasilimali zilizopo katika nchi hizo mbili.

Ameongeza kuwa hivi sasa Tanzania inafanya kazi ya kuimarisha bandari za Dar es Salaam na Tanga na kuimarisha njia nyingine za mawasiliano ili iweze kutoa huduma kwa ufanisi kwa Rwanda pamoja na nchi nyingine zinazoizunguka Tanzania na ambazo zinatengemea bandari za bahari ya Hindi katika kuagiza na kupokea mizigo kutoka nchi zilizoendelea.
Kwa upande wake Rais Kagame amesema Tanzania na Rwanda zimejidhatiti kuendeleza ushirikiano na uhusiano wa kiuchumi na kihistoria uliopo ili kuimarisha maisha ya wananchi wake.

Vile vile, Rais Kagame amemshukuru Rais Samia kwa Uongozi wake na kujitoa kwake katika kutafuta suluhu ya changamoto zinazozikabili nchi za ukanda wa Afrika Mashariki ikiwemo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Rais Kagame yuko nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo amejadili na Rais Samia masuala ya biashara, nishati na miundombinu, ulinzi na usalama pamoja na kukuza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa mataifa hayo mawili.