skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Wakati wimbi la matumizi ya madawa ya kulevya likitajwa kugharimu maisha na uchumi wa kaya na taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu ametoa wito kwa wazazi, walezi pamoja na jamii kuwajibika katika kufuatilia mienendo ya watoto ili kubaini mabadiliko hasi ya kitabia yanapojitokeza.

Rais Samia amesema hayo leo wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ambapo mamia wa wadau na wananchi walihidhuria kupata nasaha na taarifa mbalimbali kuhusu athari za matumizi ya madawa ya kulevya.

Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ahutubia katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Kupiga Vita Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya Duniani, Mkoani Arusha

Rais Samia amesema kutowajibika kwa wazazi husababisha watoto kujiunga na makundi maovu ikiwemo ulevi na matumizi ya dawa za kulevya na kujikuta wakiathirika na matumizi ya dawa hizo, hivyo ni vyema kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vilivyo kinyume na mila, desturi, maadili na silka zetu.

Rais Samia pia ameitaka jamii kuimarisha ushirikiano na viongozi wa dini pamoja na viongozi wa kijamii wakiwemo machifu kwa kuwa ndio walinzi wakuu wa maadili, utamaduni, mila na desturi.

Vile vile, Rais Samia amesema tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini na duniani kwa ujumla limekuwa likiongezeka na madhara yake ni makubwa na wakati mwingine athari zake ni za kudumu kwa jamii na kwamba mbali na kupoteza nguvu kazi ya uzalishaji, matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa kichocheo cha vitendo vya uhalifu ikiwemo wizi na unyang’anyi na hata kuambukizana maradhi kama UKIMWI na TB.

Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ashiriki Maadhimisho ya Kitaifa ya Kupiga Vita Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya Duniani, Mkoani Arusha

Kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Tanzania ilifanikiwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya kutoka nchi zinazozalisha kwa zaidi ya asilimia 90.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma