skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Ni Doto Biteko Mbunge wa Bukombe Geita, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, wadau wampa kongole

Na Veronica Simba – REA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Septemba 1, 2023 amewaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni (Agosti 30, 2023) kushika nyadhifa mbalimbali akiwemo Mhe. Dkt. Doto Biteko kwa nafasi ya Naibu Waziri Mkuu (Uratibu wa Shughuli za Serikali) na Waziri wa Nishati pamoja na Mhe. Judith Kapinga kwa nafasi ya Naibu Waziri wa Nishati.

Hafla hiyo fupi ya uapisho imefanyika Ikulu Ndogo Tunguu Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Vyama vya Siasa.

Akitoa hotuba baada ya kuwaapisha viongozi hao, Rais Samia amewataka kila mmoja kwenda kukiishi kiapo alichoapa kwa kusimama katika nafasi zao zinazowataka kuwatumikia wananchi na kujenga mahusiano mema nao.

“Kiapo mlichoapa hata Mungu anakisikia hivyo naomba mkafanye hivyo mlivyoapa,” amesisitiza na kuongeza kuwa sifa ya upole kwa kiongozi siyo ujinga bali ni maarifa.

Aidha, Mheshimiwa Rais ameeleza kuwa mabadiliko aliyoyafanya katika uteuzi wa viongozi hao siyo adhabu bali ni ya kawaida yanayolenga kuimarisha utendaji kazi Serikalini.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (kushoto) akimpongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko baada ya kuapishwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ikulu Ndogo Tunguu Zanzibar Septemba 1, 2023.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa wamewapongeza viongozi walioteuliwa na kuwataka kwenda kutimiza wajibu wao ipasavyo.

Kwa upande wao, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Janet Mbene na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy, wametoa pongezi kwa Viongozi wapya wa Wizara ya Nishati walioapishwa na kuwaahidi ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao hususan katika sekta ya nishati vijijini.

Kabla ya uteuzi, Mhe. Dkt. Biteko alikuwa Waziri wa Madini na Mhe. Kapinga ni Mbunge wa Viti Maalum (Ruvuma).

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma